Na Masanja Mabula –Pemba .24/04/2014.
Timu ya Wandishi wa Habari za
Michezo Zanzibar (ZASWA SC) imekamilisha ziara yake Kisiwani Pemba kwa
kuwafundisha soka Mavetarani wa Mji wa Chake Chake kwa kuwafunga mabao 3-1,
katika mchezo uliopigwa ndani ya dimba la Gombani .
Ushindi huo wa tatu kwa timu
ya ZASWA SC ni salamu kwa timu ambazo
zitakutana na kikosi hicho cha wanahabari kwenye michuano ya Kipwita CUP ambapo ZASWA imepangwa kundi moja na timu ya Miembeni FC.
Katika mchezo huo maveterani ndiyo walikuwa wa kwanza kuliona
lango la ZASWA Mapema dakika ya 20 kwa bao safi lililofungwa na mchezaji Ali
Kibenzi aliyeunganisha vyema krosi iliyotoka winga wa kulia.
Hata hivyo furaha ya
maveterani ilizimwa mnamo dakika ya 35 baada ya mchezaji Abdul watif kuuwahi
mpira uliotemwa na mlinda mlango wa Maveterani hao kufuatia shuti kali la
umbali wa mita 28 lililopigwa na kiungo wa ZASWA Kombo Ali Kombo .
Kuingia kwa bao hilo
kulizidisha ari kwa wachezaji wa ZASWA ambao walionekana kuutawala mchezo hali iliyosababisha washambuliaji wa ZASWA kuweka kambi ya muda
langoni kwa Maveterani hao .
Wakicheza kandanda safi ZASWA
waliongeza bao la pili katika 42 ambao liliwekwa ndani ya kamba na Kiungo
Hilali Banka baada ya kuichambua ngome ya maveterani
na kisha kuukwamisha mpira ndani ya nyavu .
Wakati akijiandaa kumpisha kiungo Khamis Dadi
kuchukua nafasi yake Kocha Mchezaji wa
ZASWA SC Ali Bakar Cheupe aliiandikia timu yake bao la tatu kunako dakika ya 76
, akimalizia pasi ya Hilali Banka aliyekuwa nyota wa mchezo huo .
Kikosi hicho cha Wandishi wa
Habari za Michezo Zanzibar kimekamilisha ziara yake Kisiwani
Pemba ambapo kimeshinda michezo mitatu kwa kuzifunga timu za Wilaya ya
Wete , Mkoani n Chake Chake huku kukipoteza mchezo katika Wilaya ya Micheweni .

EmoticonEmoticon