Waasisi
wa Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar, Hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (kushoto) na Hayati, Abeid Aman
Karume (kulia waliokaa) wakisaini nyaraka muhinchi za Hati
za Muungano mwaka 1964 (mada ya historia).
******************************
''WASOMI
NA WANASIASA WAKONGWE NINYI NDIYO HASA TEGEMEO LA KWELI KWA VIJANA WA
KIZAZI KIPYA KWA KUMBUKUMBU MLIZONAZO KUHUSU SUALA ZIMA LA TANGANYIKA NA
ZANZIBAR, BADALA YAKE MNAWALISHA SUMU VIJANA ILI KUAMINI KILE
MNACHOKIELEZA MBELE YA JAMII, MNAHISI NINI KITATOKEA IWAPO VIJANA WA DOT
COM WAKIAMINI MNACHOKIPIGIA DEBE???? BADALA YA KUUELEZA UMMA UKWELI NA
KUJENGA HOJA YA HAJA ILI MUWEZE KUELEWEKA''.
Rais
Julius Kambarage Nyerere, akichanganya udongo wa Tanganyika na
Zanzibar, huku akishuhudiwa na Rais wa Zanzibar, Abeid Aman Karume, (wa
tatu kushoto) na Mhe. Rashind Mfaume Kawawa (wa kwanza kulia) wakati wa
sherehe za kwanza za Muungano zilizofanyika Tarehe 26 APRIL, 1964.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (kushoto)
na Sheikh Abeid
Amani Karume (kulia) wakibadilishana Hati
za Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar mwezi Aprili, 1964.
Walioshiriki katika tukio la kuchanganya udongo wa Tanganyika na
Zanzibar tarehe 24 Aprili, 1964 wakiwa katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam
wakati wa halfa fupi ya sherehe za miaka 48 ya Muungano tarehe 26 Aprili, 2012.
Kutoka kushoto ni Bi. Khadija Abasi
Rashid, Bw. Elisaeli Mrema, Bw. Hassan Omari Mzee na Bi. Sifael Mushi.
Rais Julius K. Nyerere (katikati),
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar Mhe. Abeid
Amani Karume wakukagua gwaride wakati wa maadhimisho ya sherehe za Muungano
zilizofanyika Zanzibar mwaka 1966.
*********************************************
TAMKO LA SERIKALI KUHUSU HATI ZA MUUNGANO
TAREHE
14 APRILI, 2014 __________________________________________________
Siku 12 zijazo tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamezaliwa watu
ndani ya Muungano huu na wengine wana wajukuu.
Inasikitisha sana
kuwa leo, miaka 50 baadaye ipo dhana potofu inayojengwa kuwa Muungano huu si
halali kwa vile hakuna Hati ya Muungano (Articles of the Union).
Waasisi wa Taifa letu ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule Zanzibar walitia
saini Hati hiyo, mbele ya mashuhuda, nao wameonekana kama walichokifanya
kilikuwa kiini macho, na kwa hiyo kwamba waliongoza Taifa jipya la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa msingi wa kiini macho hicho kwa miaka yote hadi
Mwenyezi Mungu alipowaita.
Mambo yote mawili yametusononesha sana
sisi Serikalini, na bila shaka yamewasononesha wananchi wanaoipenda nchi yao,
wanaowapenda Waasisi wa Taifa letu na kuuenzi Muungano wao.
Madai
ya kuonyeshwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi lakini hatukuweza kuamini hali
itafikiwa ilipofikia, ambapo wapo watu wanathubutu kudai na kuapa kuwa Hati
hiyo haipo.
Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote.
Hata hivyo, lazima tukubaliane kuwa zipo Hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo
wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama
mboni ya jicho.
Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka
1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na Hati ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.
Hati za aina hii zinahifadhiwa maeneo
maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi,
tunazifungua ili kuzihifadhi kwa namna yoyote ile. Lakini sasa
maneno yanakua mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi
cha wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo kweli Hati ya Muungano ipo au la.
Hivyo, kwa maagizo na ridhaa ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninaleta mbele yenu Hati ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume, ili muione na
kuwahakikishia Watanzania kuwa yanayosemwa kuwa hakuna Hati hiyo si kweli.
Hati
hiyo ipo tangu wakati huo, imetunzwa vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na
tutaendelea kuihifadhi. Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti
wa Bunge Maalum nina uhakika Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala
wa kama Hati ipo au la.
Isitoshe, tufanye utaratibu wa kuweka
nakala kwenye Makumbusho ya Taifa ili kila atakayetaka kuiona katika miaka
mingine 50 ijayo na kuzidi aione.
Mwisho, narejea kusema kuwa kwa
upande wa Serikali tunasikitishwa na kufadhaishwa sana na tuhuma nzito kwamba
labda waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia wawepo
Watanzania wenzetu, wafikie hapo. Ni jambo zito. Vile vile
hatukutarajia kuwa Serikali itatuhumiwa kuwa haikuwa makini kuhifadhi
waliosaini waasisi wetu.
Matumaini yetu ni kuwa baada ya leo
tutaendelea na mambo ya msingi kwa mustakabali, umoja na uimara wa Taifa letu
badala ya kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna msingi imara wa kisheria.
Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, DAR ES SALAAM.
14 Aprili, 2014
EmoticonEmoticon