WADAU JITOKEZENI KUISADIA AFC YAKUMBWA NA UKATA WA ELA

April 23, 2014

picha na maktaba 
MABINGWA wa soka Mkoa wa Arusha, AFC, huenda ikashindwa kushiriki vema Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL), inayotarajiwa kuchezwa kwa mkondo mmoja katika vituo vitatu vya timu tisa kila kimoja kuanzia Mei 10 kutokana na ukata unaoikabili.
Kutokana na hali hiyo, wadau wa soka mkoani hapa wametakiwa kuacha tofauti zao na kujiunga pamoja kuisaidia AFC ili iweze kufufua matumaini ya kurejea Ligi Kuu Tanzania bara baada ya kuwa nje kwa miaka minne.
AFC ni kati ya timu kongwe nchini na iliwahi kutamba Ligi Kuu tangu ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza na iliwahi kufanya vizuri hadi kushiriki Ligi ya Muungano miaka ya tisini kabla ya kupoteza uelekeo na hatimaye kushuka daraja.
Meneja wa AFC, Denis Shemtoi, alikiri timu kuwa katika wakati mgumu, ingawa wana imani kuwa jitihada zao za kusaka wahisani na wafadhili zitazaa matunda, kwani baada ya timu kufanikiwa kutwaa ubingwa wa mkoa, baadhi ya waasisi na wapenda soka wameanza kujitokeza kufuatilia maandalizi ya timu, hivyo huo ni mwamko mzuri.
Shemtoi alisema kuwa kwa sasa timu inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta na jitihada za kufanya usajili zimefanikiwa na lililoko mbele ni kusaka mechi za majaribio kupima uwezo wa kikosi hicho ili kuwavutia wadau na kuwahamasisha kuichangia.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), Amir Mhando, amekuwa mstari wa mbele kukusanya wadau wa soka ili waweze kuunda kamati ya kusaidia AFC irejee Ligi Kuu, jitihada ambazo zimeanza kuzaa matunda ingawa bado hali si njema.
Mkoa wa Arusha umejikuta ukikosa Ligi Kuu mwakani baada ya JKT Oljoro kushuka msimu huu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ameahidi kusapoti jitihada za wapenda kandanda mkoani hapa, kama watataka msaada kutoka ofisi yake, kwani sera za Tanzania zinasapoti michezo huku akiwataka wahusika wajipange vema na kuonyesha wazi dhamira zao.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »