VPL: ASHANTI VS MBEYA CITY, YANGA VS JKT RUVU NI MITANANGE MIZITO ZAIDI WIKIENDI HII, MECHI YA SIMBA, KAGERA HAINA `PRESHA`!!
Na Baraka Mpenja .
LIGI
kuu soka Tanzania bara inatarajia kuendelea kesho na keshokutwa, huku
mechi kubwa yenye uzito wa hali ya juu ni kati ya Yanga dhidi ya JKT
Ruvu na ile ya Ashanti United na Mbeya City.
Kesho
jumamosi zitapigwa mechi mbili ambapo wauza mitumba wa Ilala
watawakaribisha Mbeya City katika dimba la Azam Complex, Chamazi, nje
kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mechi hii itakuwa na mvuto wake kutokana na mazingira ya timu zote mbili katika msimamo wa ligi hiyo.
Mbeya City wapo nafasi ya tatu wakiwa wameshuka
dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 45, pointi moja nyuma ya mabingwa
watetezi Yanga waliopo nafasi ya pili kwa pointi 46 baada ya kucheza mechi 22.
Kocha Juma Mwambusi ataingia kesho kwa lengo la kutafuta
ushindi ili kujiongezea pointi katika harakati zake za kuwania ubingwa wake wa
kwanza msimu huu.
Mbeya City ni timu pekee iliyofanya vizuri na
kuwashangaza wapenzi wa soka kati ya klabu tatu zilizopanda ligi kuu msimu huu
unaoelekea mwishoni.
Wenzao, Ashanti United na Rhino Rangers wapo katika
hatari ya kushuka daraja, lakini maafande wa Tabora wanaonekana kwa asilimia
kubwa wameshashuka daraja.
Ashanti wameshuka dimbani mara 23 na kujikusanyia
pointi 21 katika nafasi ya 12, wakati Rhino Ranger ndio wanaoburuza mkia kwa kuwa
na pointi 13 katika nafasi ya 14 baada ya kucheza mechi 23.
Katika mchezo wa kesho, kocha mkuu wa Ashanti
United, Abdallah Kibadeni hahitaji matokeo mengine yoyote zaidi ya ushindi
kwasababu akipoteza mchezo atazidi kujiweka mazingira magumu zaidi ya kubakia
ligi kuu.
Lakini atahitaji kuwa na mipango mizuri zaidi mbele
ya Wagonga nyundo, kwasababu umoja walio nao na uwezo wa kikosi chao, wanaweza
kuibuka na ushindi.
Kule Kaitaba kutakuwa na mchezo mmoja kesho jumamosi
ambapo wenyeji Kagera Sugar watakuwa wanachuana na Simba sc ya jijini Dar es
salaam.
Simba sc wanaingia katika mchezo wa kesho wakiwa
hawana cha kupoteza, kwasababu hawahitaji ubingwa wala nafasi ya pili.
Hata hivyo ushindi ni muhimu kwao ili kulinda
heshima yao inayozidi kupotea siku za karibuni.
Wataingia uwanjani wakiwa wamepoteza mechi mbili
zilizopita dhidi ya Coastal Union na Azam fc, hivyo kupoteza mechi ya kesho ni
kuwatonesha zaidi kidonda mashabiki wao.
Simba mpaka sasa wapo nafasi ya 4 katika msimamo
baada ya kucheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 36.
Kagera Sugar wao wanahitaji nafasi ya tatu au nne
msimu huu, hivyo kesho wataingia kutafuta pointin tatu muhimu.
Kagera kwasasa wapo nafasi ya 5 wakiwa na pointi 33
baada ya kucheza mechi 22.
Ligi hiyo itandelea tena jumapili (aprili 6) ambapo mechi kali ni baina ya mabingwa
watetezi, Yanga dhidi ya JKT Ruvu uwanja
wa Taifa.
Umuhimu wa ushindi kwa timu zote mbili ndio sababu
ya mchezo huo kuwa na mvuto kwa mashabiki wa soka.
Yanga wanahitaji matokeo kwa njia zote ili kupunguza
pengo la pointi na vinara Azam fc wenye pointi 53 kileleni.
Wanajangwani hao wameshuka dimbani mara 22 na
kujikusanyia pointi 46 katika nafasi ya pili, na nyuma yao wapo Mbeya City
wenye pointi 45.
Yanga wanahitaji kutetea ubingwa wao walioweka
rehani mbele ya Azam fc, hivyo kushinda kesho ni muhimu zaidi kwasababu mechi
iliyopita walifungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Kule Tanga.
Nao JKT Ruvu chini ya kocha mkuu Fredy Ferlix
Minziro wanahitaji pointi tatu muhimu ili kuendelea kujiimarisha katika
mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Kwasasa wapo nafasi ya 9 kwa pointi 28 baada ya
kucheza mechi 23, hivyo ushindi katika mechi hiyo utakuwa na maana kubwa kwao.
Matokeo yamekuwa magumu kuyatabiri kwa sasa, timu
yoyote inaweza kushinda bila kujali ubora na majina ya wachezaji kutofautiana.
Mechi nyingine za jumapili ni kati ya Coastal Union
dhidi ya Mgambo uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Vibonde JKT Oljoro watakuwa na kibarua muhimu na
maafande wa jeshi la Magereza kutoka jijini Mbeya, Tanzania Prisons
`Wajelajela` katika dimba la Shk. Amri Kaluta Abeid jijini Arusha.
Rhino Ranger waliopoteza matumaini ya kubakia ligi
kuu watawakaribisha, Mtibwa Sugar kutoka Marogoro kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
mjini Tabora.
Mechi ya Ruvu Shooting na Azam iliyotakiwa kupigwa jumapili imesogezwa mbele mpaka aprili 9 mwaka huu kwasababu wachezaji wengi wa Azam fc wameondoka na kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes.
EmoticonEmoticon