MJUMBE
wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Mark Mwandosya ameomba Bunge
Maalumu la Katiba, kukata posho ya siku moja ya wajumbe wote wa Bunge
hilo ili kuwapa pole waathirika wa mafuriko nchini, ikiwa ni pamoja na
viongozi waliopata ajali ya helikopta.
Profesa
Mwandosya alitoa pendekezo hilo kwa Bunge, baada ya Mwenyekiti wa
Bunge hilo, Samuel Sitta kutoa taarifa ya maendeleo ya afya za viongozi
waliopata ajali ya helikopta jijini Dar es Salaam wakati wakitathimini
maafa ya mafuriko hayo.
Alisema
wanaendelea vizuri. Baada ya taarifa hiyo, Profesa Mwandosya aliomba
mwongozo wa Mwenyekiti na kutoa pendekezo hilo la kutaka Bunge kukata
posho ya siku moja ya wajumbe wote kutoa pole kwa waathirika wa
mafuriko hayo.
Akijibu
mwongozo huo, Sitta alisema kwa vile suala hilo lilikuwa
halijajadiliwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge, isingekuwa rahisi kwake
kukubaliana au kukataa pendekezo hilo na hivyo alisema ataliwasilisha
kwenye Kamati hiyo kupata uamuzi.
Katika
hatua nyingine, Sitta amesema mjumbe yeyote wa Bunge hilo ambaye
ataona hatendi haki katika uendeshaji wa Bunge hilo kuwasilisha
malalamiko yake kwa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
Aliyasema
hayo bungeni mjini hapa jana wakati akijibu mwongozo wa Mjumbe wa
Bunge hilo, Dk Hamisi Kigwangala aliyemtuhumu Sitta kuwa anafanya
upendeleo katika uendeshaji wa bunge hilo kwa kuwapendelea wajumbe
walio wachache.
Kigwangala
alisema kwa vile Sitta alimpa nafasi maalumu Msemaji wa walio wachache
wa Kamati Namba Nne, Tundu Lissu kutoa ufafanuzi baada ya kukatika
matangazo ya TBC 1 Jumamosi, yeye pia anastahili kupewa nafasi hiyo kwa
vile matangazo yalikatika akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo.
Akijibu
mwongozo huo, Sitta alisema alimwagiza Katibu wa Bunge kufuatilia.
“Baadaye Katibu wa Bunge alinitaarifu kuwa baada ya kuwasiliana na watu
wa TBC 1 na walipofuatilia namna matangazo hayo yalivyokuwa yakirushwa
hawajabaini kama kuna mahali yalikatika wakati Dk Kigwangala
akizungumza, hivyo hoja yake ikakosa nguvu,” alisema Sitta.
EmoticonEmoticon