MWANDISHI ANUSURIKA, MTOTO MCHANGA AOKOLEWA

April 23, 2014

 Mgambo aliyetaka kumtwisha Nyundo mtoto Anna Yohana, akimbeba mtoto akiwa na hofu kuwa amemdhuru vibaya....
 Mtoto Anna Yohana aliyenusurika kuuawa kwa nyundo na Mgambo wa Jiji la Mbeya, akiwa amebebwa na msamaria mwema, baada ya mwandishi Gordon Kalulunga, kusogea na kuwapiga picha Mgambo wakashituka na kuanza kumshambulia kisha oparesheni ikaahirishwa.
 Baada ya kujinasua na kupigana na mgambo zaidi ya saba, nikipiga simu kwa baadhi ya waandishi wa habari huku Tape recorder ikiwa imeporwa.
 
 
*Ni kichanga cha miezi minne kilichofunikwa kwenye salfeti sokoni.
*Wauza magazeti nao wahaha meza zao kuvunjwa usiku wa manane.
 
Na,Christopher Nyenyembe, Mbeya
 
MWANDISHI wa Habari wa Gazeti hili (Tanzania Daima) mkoa wa Mbeya, Gordon Kalulunga, ameambulia kipigo kutoka kwa mgambo wa jiji alipokuwa kazini akipiga picha kwenye ‘operesheni vunja vunja’ sehemu ambayo mtoto mchanga wa miezi minne alikuwa amelazwa na mama yake mzazi kwenye salfeti  sokoni eneo la Kabwe Mwanjelwa.
 
Tukio hilo lilitokea wakati wa sherehe za pasaka(jumatatu ya pasaka) baada ya uongozi wa jiji la Mbeya kwa kutumia mgambo wake walipoamua kuendesha operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara waliopanga bidhaa zao kando kando ya barabara kuu ya Tanzania- Zambia katika eneo maarufu la Mwanjelwa.
 
Mwandishi Kalulunga alikutwa na mkasa wa kupigwa na mgambo zaidi ya saba na kusababisha purukshani kubwa mara alipofanikiwa kupiga picha zilizowahusu mgambo hao waliokuwa wakivunja vibanda na kuwatimua wafanyabiashara ndogo ndogo waliopigwa marufuku kupanga bidhaa zao kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwa lengo la kuweka usafi wa jiji hilo.
 
“Nilikuwa natimiza wajibu wangu wa kazi kama mwandishi wa habari,alitokea mwanamke  mmoja aliyekuwa amevaa gauni refu la rangi ya njano na kunikaba shati,ndipo mgambo wa jiji walipokuja na kuanza kunipiga,ilibidi kamera yangu nimkabidhi polisi mmoja lakini nimepoteza redio yangu ya kurekodia”alisema Kalulunga.
 
Alisema baada ya tukio hilo kutokea ilibidi akatoe taarifa kwenye kituo kidogo cha polisi Mwanjelwa na kupewa fomu ya kwenda kutibiwa (PF 3) ambako ilibidi apatiwe matibabu na aliporudi polisi Mwanjelwa alitakiwa na mkuu wa kituo hicho akatoe maelezo yake kituo kikuu cha polisi mjini kwa OC –CID au mkuu wa polisi wilaya (OCD).
 
Kitendo cha Mwandishi huyo kushambuliwa akiwa kazini kulisababisha habari za haraka zisagae jijini humo na kisha kumfikia Kamanda wa Polisi mkoa huo,Ahmed Msangi aliyeongea moja kwa moja na Kalulunga ili aweze kufahamu aina ya uvunjifu wa amani uliojitokeza wakati wa operesheni vunja vunja iliyokuwa akifanywa na mgambo hao ambao imechangia pia kuvunjwa vibanda vya kuuzia magazeti tangu zoezi hilo lilipoanza.
 
“Namshukuru sana mkuu wa polisi wilaya ya Mbeya,Richard Mchomvu ametumia busara kubwa sana kunikutanisha na kiongozi wa operesheni hiyo kutoka idara ya afya aliyejulikana kwa jina la Odas na mkuu wa mgambo pamoja na bosi wangu kazini,jiji wamekiri kunifanyia kitendo hicho eti walikuwa hawafahamu kama mimi ni mwandishi” alisema Kalulunga.
 
Kufuatia tukio hilo lililotulizwa na Mchomvu aliushauri uongozi wa jiji hilo kushirikiana na vyombo vya habari katika majukumu yake kwa kuwa  wananchi wanapaswa kuelimishwa zaidi kila jambo linapofanyika na kusisitiza kuwa usafi wa jiji ni muhimu hivyo kila upande una jukumu lake hivyo hawana sababu yoyote ya kuonyeshana ubabe.
 
“Nikiwa mkuu wa polisi wa wilaya sipendi kuona haki za binadamu zikivunjwa kienyeji,uhai wa kila mtu ni muhimu zaidi,tumieni vyombo vya usalama kuweka mambo yenu vizuri,waandishi nao wana jukumu kubwa la kuwasaidieni watumieni,angalieni sasa mmepoteza kifaa chake cha kazi,naomba suala hili mlimalize kwa ustaarabu hata Mkurugenzi anapaswa kujua” alisema Mchomvu.
 
Kufuatia tukio hilo na mtoto mchanga aliyenusurika kupigwa nyundo wakati mgambo hao wakiendelea kubomoa vibanda,operesheni hiyo ilisitishwa mara moja katika eneo hilo baada ya mama mzazi wa mtoto huyo alipofanikiwa kutimua mbio na kumuacha mwanae aliyeangukia kwenye mikono ya wasamaria.
 
Wakati hali hiyo ikitokea,wauzaji wa magazeti jijini humo wamelalamikia zoezi hilo ambalo limewasababishia  hasara kubwa baada ya meza zao kuvunjwa usiku wa manane wakati uongozi wa jiji hilo unafahamu fika aina ya meza zilizoruhusiwa kuwepo kwa ajili ya kuuzia magazeti na haijulikani mahali zilipotupwa.
 
Jiji la Mbeya limekubali kulipa kifaa kilichoibwa/kupotea katika tafrani hiyo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »