KMKM BINGWA MPYA LIGI KUU ZANZIBAR

April 06, 2014
Na Abdi Suleiman, Pemba
KMKM imeweza kutetea taji la ubingwa wa soka Zanzibar, baada ya leo jioni kuikong’ota Chipukizi mabao 3-2 katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu ya Grand Malt Zanzibar 2013/2014 uliopigwa uwanja wa Gombani Pemba.
 
Mabaharia hao wanapaswa kuishukuru pia timu ya Jamhuri ambayo iliilaza Polisi bao 1-0 katika uwanjawa Amani, na kuwasafishia njia washika magendo hao kulipeleka tena kombe la ubingwa makao makuu yao mtaa wa Kibweni.
 
Kwa ujumla mchezo kati ya KMKM na Chipukizi ulikuwa mzuri na uliojaa msisimko, na haikuwa rahisi kutabiri mshindi hadi dakika 15 za mwisho.



MAKAMU Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) Khamis Abdalla Said, akimkabidhi kombe la ubingwa wa ligi kuu ya soka Zanzibar Grand Malt, Mwnyekiti wa KMKM Khamis Khatib, katika uwanja wa Amani jioni hii baada ya timu hiyo kuishinda Chipukizi mabao 3-2 Gombani Pemba. (Picha na Ameir Khalid).   

KMKM ilianza kucheka na nyavu katika dakika ya 15 kupitia mshambuliaji wake Maulid Kapenta, ambalo lilidumu hadi wakati wa mapumziko.
 
Kipindi cha pili, mashua za KMKM ziliongeza kasi na kufanikiwa kuandika bao la pili lililofungwa na Mudrik Muhibu dakika ya kuongeza la pili kwenye dakika ya 59.
 
Kuona hivyo, Chipukizi ilicharuka na ikamudu kurejesha mabao hayo katika dakika ya 65 na 76 mtawalia yote yakifungwa na Faki Mwalimu kabla Juma Mbwana kuipachikia KMKM bao la tatu na la ushindi.
 
Naye Ameir Khalid, anaripoti kutoka uwanja wa Amani kuwa bao pekee lililofungwa na mchezaji Abdulatif Omar katika dakika ya 36, lilitosha kuinyima Polisi iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa, kuipokonya KMKM ubingwa.
 
Wawakilishi wa KMKM waliokuwepo uwanja wa Amani walikabidhiwa kombe hilo la ubingwa wa ligi hiyo inayodhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt.
 
Leo usiku, wadhamini wa ligi hiyo wanaandaa tafrija maalumu kuzipongeza timu shiriki na wadau wote wa soka waliofanikisha ligi hiyo inayoidhamini kwa msimu wa pili sasa.   

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »