KATIBU MWENEZI WA CHADEMA JIJI LA MBEYA AACHIA NGAZI.

April 23, 2014

Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Mbeya,Bwa.Lucas Mwampiki.
=======  ======  =======
SIKU mbili baada ya aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Jiji la Mbeya Lucas Mwampiki kutangaza kujiuzulu wadhifa wake, chama hicho kimedai kuwa kilishamvua nafasi hiyo kabla hajatangaza kujiuzulu kutokana na kuvujisha siri za chama kwa upinzani.

Mwampiki ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwakibete alitangaza kujiuzulu nafasi ya Katibu Mwenezi kwa madai kuwa amekuwa akitengwa na baadhi ya viongozi wa chama katika shughuli mbalimbali za chama kwa nafasi yake kama mjumbe.

Akitangaza uamuzi wa chama hicho dhidi ya Mwampiki, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya mjini John Mwambigija alisema kuwa kikao cha kumvua uongozi Katibu Mwenezi huyo kiliketi April 14 baada ya kujiridhisha mwenendo wa utendaji wake na  yeye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo April 16.

Alisema kuwa kufuatia hali hiyo uongozi wa chama wilaya kwa kuhusisha vikao halali vya chama umeridhia kumuengua katika nafasi yake ikiwa ni pamoja na kumzuia kutojihusisha na shughuli zozote za chama.

Mwambigija alisema kuwa kiongozi  huyo wa juu wa chama alikiuka vifungu vya katiba ya chama kwa kusambaza taarifa za majungu na kutokuwa mkweli na muwazi ikiwa ni pamoja na kujihusisha na upotoshaji juu ya maamuzi halali ya chama.

‘’Tumeamua kwa kauli moja kumsimamisha shughuli zote za chama kwa mwaka mmoja,ataendelea na Udiwani wake, hatakiwi kufanya chochote kinachohusiana na chama chetu,akiendelea tutachukua uamuzi wa kumnyang’anya kadi na kumvua uanachama,’’alisema Mwambigija.

Alifafanua kuwa miongoni mwa sababu zilizosababisha avuliwe wadhifa wake ni pamoja na kuvujisha siri za chama kwa wapinzani ikiwa ni pamoja na kutotoa ushirikiano katika harakati za chama za sasa za ‘Chadema ni Msingi’ na kwamba uamuzi waliouchukua uko katika sheria zinazolindwa na Katiba ya chama.

Alisema kuwa kabla ya kuchukua uamuzi huo chama kilimuita kiongozi huyo katika vikao mara nne ambapo alishindwa kuhudhuria hivyo uamuzi waliouchukua una baraka za vikao halali vya chama na kuwa hata hivyo anayo nafasi ya kukata rufaa kwa ngazi za juu iwapo ataona kuwa hajatendewa haki dhidi ya uamuzi huo.

Kwa upande wake Katibu Mwenezi aliyejiuzulu Mwampiki alisema kuwa aliamua kujiuzulu baada ya kuona hapewi ushirikiano na viongozi wenzake na kuwa mara nyingi alipokuwa akihoji mambo ya msingi ya kukiendeleza chama amekuwa akinyooshewa kidole kama msaliti.

‘’Nimeamua kujiuzulu mwenyewe bila kushinikizwa na mtu, kutokana na afya ya chama, kwa mujibu wa Katiba ya chama ya mwaka 2006 kifungu 6.3.4(a) hiki kinaainisha ukomo wa uongozi, nimetumikia chama kwa kila hali hadi rasilimali fedha, nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu,’’alisema Mwampiki.

Aidha alisema kuwa hajawahi kuitwa na viongozi  wala kuandikiwa barua yoyote inayomtaka kufika ofisini ambayo kulingana na taratibu ilipaswa kumfikia ndani ya siku 14 na yeye kuweka saini yake hivyo uamuzi wowote uliochukuliwa dhidi yake ulipaswa kuzingatia taratibu hizo.

‘’Siwezi kuchukuliwa hatua bila maandishi ambayo yanapaswa kunifikia ndani ya siku 14, vinginevyo uamuzi wowote dhidi yangu mbali na kutamka kujiuzulu kwangu, haujafuata taratibu za kisheria,’’alisema Mwampiki.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »