Dar es Salaam. Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania imeungana na maaskofu mbalimbali kuwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kuheshimu Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa kwa mujibu wa sheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia, taasisi hiyo imemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kujiuzulu nafasi
zake zote za uongozi kutokana na kauli waliyodai ya kichochezi,
aliyoitoa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma kuwa ukipitishwa
muundo wa serikali tatu, jeshi litachukua nchi kwa sababu itashindwa
kuwalipa mishahara.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji
wa Jumuiya na Taasisi hizo, Sheikh Rajab Katimba alilaani kauli kuhusu
jeshi na kuwa makanisa yote yatafungwa na nchi itakosa amani kutokana na
kupitisha muundo huo wa serikali.
Sheikh Katimba alisema Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba imetokana na utafiti na uchambuzi wa maoni
ya wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani ili kuboresha Muungano kutatua
kero zilizodumu kwa miaka 50 sasa.
Msimamo
Jumuiya hiyo iliweka wazi msimamo wake wa kutaka
serikali tatu na kutaka maoni ya makundi mbalimbali ndani ya Bunge la
Katiba kuheshimiwa.
Mjumbe wa Jumuiya hiyo, Sheikh Ramadhan Sanze pia alisema si ustaarabu kwa kundi moja kuhodhi mchakato kwa masilahi binafsi.
Alisema kukosoa maoni ya waasisi wa Taifa si
dhambi kwa sababu wao hawakuwa Mungu kwamba hawakosei, badala yake
alipendekeza watu waachwe wazungumze kwa utashi wa matakwa yao juu ya
kile kilichowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Nchi hii haithamini mchango wa wataalamu, tumeona
Tume ilivyofanya kazi nzuri, leo hii wanatukanwa hadharani, nawashangaa
sana viongozi wa nchi hii,” alisema.
Sheikh Sanze alisema miiko na misingi waliyoiweka
waasisi wa Taifa inavunjwa na viongozi wenyewe ambao leo wanasema
waasisi wanatukanwa kwa kuwa wamependekeza serikali tatu badala ya mbili
walizounda waasisi.
“Kulikuwa na utaratibu wa kubadilishana awamu za
uongozi katika Serikali ya Muungano, awamu hii rais akitoka Tanzania
Bara, ijayo atatoka Zanzibar; hii ndiyo misingi waliyoiweka waasisi,
mbona leo haifuatwi? Huu ni unafiki...” alifafanua Sheikh Sanze.
Jumuiya hiyo imewataka wananchi wote kuendelea na
mshikamano katika kutengeneza Katiba Mpya yenye maridhiano na
itakayoondoa kero zilizodumu kwa zaidi ya miaka 50.
chanzo:Mwananchi
chanzo:Mwananchi
EmoticonEmoticon