January 10, 2014

YANGA SC WAKUTANA NA ROBERTO CARLOS UTURUKI

Na Baraka Kizuguto, Antalya

WACHEZAJI wa Yanga SC wamepata fursa ya kukutana na beki wa zamani wa kimataifa wa Brazil, Roberto Carlos ambaye kwa sasa ni kocha wa klabu ya Sivasspor iliyopo Ligi Kuu nchini hapa.
Yanga imefikia katika hoteli ya Sueno Beach Side eneo la Manavgat pembeni kidogo ya jiji la Antalya leo asubuhi imeanza mazoezi ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Roberto Carlos katikati akiwa na Mkwasa na Nizar kushoto

Timu ilipokelewa na wenyeji majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za huku ikiwa ni sawa na saaa 12 kwa saa za Afrika Mashariki na moja kwa moja kikosi kilielekea katika mji wa Manavgat ambapo ndipo ilipo hoteli ya Sueno Beach Side ambapo msafara mzima umefikia.
Sueno Hotel Beach Side ni hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano, ambayo ina jumla ya vyumba 760, mabwawa ya kuogelea,viwanja viwili vya mpira vya mazoezi kimoja kikiwa na nyasi za kawaida na kingine nyasi za bandia.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema anashukuru kikosi chake kimefika salama na wachezaji wote wakiwa katika hali nzuri kiafya na kifikra hivyo anatarajiwa mazoezi yatakayoanza leo yatasaidia kuiweka timu katika hali nzuri na kuwa tayari kwa mashindano.
Wachezaji wa Yanga katika picha ya pamoja na Carlos
Kulia Juma Pondamali na kushoto Baraza Kizuguto wakiwa na Carlos
Wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi


"Kazi yangu kubwa ni kukiandaa kikosi kiwe katika hali nzuri ili pindi tutakaporejea nchini timu iwe fiti na tayari kwa ajili ya mashindano, kwa hali ilivyo nzuri na mazingira naamini timu itabadilika na kurejea nchini ikiwa katika kiwango cha kizuri cha ushindani" alisema Mkwasa
Yanga inatarajia kucheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya timu ya Ankara Sekerspor iliyopo Ligi Daraja la Kwanza nchini Uturuki.
Aidha timu ya Sivasspor pia imeweka kambi katika hoteli ya Sueno na leo asubuhi kabla ya Yanga kuanza mazoezi waliweza kupiga picha ya pamoja na gwiji huyo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »