MWANAJESHI FEKI ATIWA MBARONI AKIMTAPELI DC

January 21, 2014
 'Koplo' feki akichukuliwa maelezo na Luteni Yahya Wangwe na Mteule daraja la pili Albano Semfuko.
 
Na Mashaka Mhando,TANGA 
VIKOSI vya Ulinzi na Usalama Wilayani hapa,vinamshikilia Edwin John Mponji (31) kufuatia kwenda ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tanga na kujitambulisha kwamba yeye ni koplo wa jeshi la Wananchi JWTZ akitaka kijana wake afanyiwe mpango wa kuingizwa Jeshi la kujenga Taifa.

 "Koplo" Mponji alikwenda ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tanga,Halima Dendego Januari 16 mwaka huu siku ambayo Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilayani hapa ilikuwa katika zoezi la kuwafanyia usaili vijana wanaotakiwa kujiunga na jeshi la kujenga Taifa (JKT).

Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya,Mponji alijitambulisha kuwa yeye ni afisa wa JWTZ ambaye kwa sasa yupo kikosi cha 36 KJ Mkoani Pwani ambapo aliambatana na kijana Emmanuel Joseph akitaka afanyiwe mpango ili apate nafasi.

Hata hivyo wakati akitoa maelezo hayo,Mshauri wa Mgambo wa Wilaya ya Tanga,Sir Meja Albano Semfuko alimtilia shaka na kumjulisha Mkuu wa Wilaya ambaye aliamuru ashikiliwe kwa mahojiano zaidi. Akizungumza na waandishi wa habari,Mkuu wa Wilaya ya Tanga alisema baada ya mahojiano ilibainika kuwa Mponji sia askari wa JWTZ ndipo akalazimika kupelekwa nyumbani kwake mtaa wa Magomeni Jijini hapa alipopekuliwa alikutwa na sare za JWTZ zikiwa na cheo cha koplo.

Alisema wakati akikamatwa,Mponji alikuwa amevaa kaptura ya jeshi la Polisi lakini alipowekwa rumande ya kituo cha Polisi Chumbageni alifanya njama za kuivua na kisha kumpa mahabusu aliyekuwa akitoka ambaye alitoweka nayo.

Mponji alionyeshwa kwa waandishi wa habari akiwa amevalia sare ya jeshi la Wananchi ambapo alipohijiwa alishindwa kutoa maelezo ya kueleweka juu ya wapi alikokuwa amezipata sare hizo inagawa alikiri kuwa aliwahi kumaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kikosi cha 841 KJ Mafinga. 

Kufuatia tukio hilo,Mkuu wa Wilaya ya Tanga aliamuru Jeshi la Wananchi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kumfanyia uchunguzi wa kina ili kubaini mtandao wake.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »