📌Apongeza jitihada za kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi
📌Awataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kushirikiana na TANESCO kulinda miundombinu ya umeme
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amelipongeza Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kwa kufanya maboresho makubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na kuendelea kusogeza huduma zake karibu wananchi.
Akizungumza Novemba 20 wakati akifungua kikao kazi kati ya TANESCO, madiwani na wenyeviti wa Serikali za mitaa kutoka Halmashauri za Manispaa ya Ilala, Temeke na Kigamboni, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Mpogolo amebainisha kuwa viongozi hao ni nguzo muhimu katika kufikisha taarifa, kero na changamoto za wananchi kwa Taasisi husika.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa viongozi hao katika kusimamia ulinzi wa Miundombinu ya Umeme, kwani Serikali imewekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya umeme ambayo inapaswa kuendelea kuwanufaisha wananchi kijamii na kiuchumi.
“Kikao kazi hiki kinawapa nafasi Wenyeviti wa Serikali za Mitaa pamoja na Madiwani kutambua kazi kubwa inayofanywa na TANESCO kwa nchi yetu, ikiwa ni pamoja na kuwaweka karibu viongozi hao na TANESCO katika kushirikiana na wananchi katika suala zima la utumiaji wa huduma za umeme na ulinzi wa miundombinu ya umeme.
"Nachukua nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO pamoja na Serikali kwa ujumla kwa uwekezaji mkubwa katika miradi ya umeme ambayo imekuwa na manufaa chanya kwa wananchi kiuchumi na kijamii,” alisisitiza Mhe. Mpogolo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bi. Irene Gowelle, amesema TANESCO inaendeleza mkakati wa kufanya kazi kwa karibu zaidi na Viongozi wa Serikali za mitaa ili kuwafahamisha kuhusu maboresho yanayoendelea kufanyika pamoja na maendeleo ya miradi ya umeme katika maeneo yao. Pia kuwaweka karibu viongozi hao kuwafanya kuwa kiungo muhimu katika kupeleka taarifa kwa wananchi.
“Serikali sasa imeelekeza kuongeza nguvu katika kuwahudumia wananchi hivyo Ushirikiano na viongozi hawa ni muhimu kwa kuwa wao daraja kati yetu na wananchi kwenye maeneo yao na tukifanya nao kazi kwa ukaribu, tutawafikia wananchi kwa haraka na kwa uhakika zaidi,” alisema Bi. Gowelle.
Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Abbas Mwegamno, ameishukuru TANESCO kwa kutoa nafasi kwa viongozi hao kushiriki katika kikao kazi hicho na kuwapa elimu kuhusu miradi ya umeme. Amesema hatua hiyo inawajengea uwezo wa kurudisha taarifa kwa wananchi, kama inavyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu wajibu wa mamlaka za umma.
Miongoni mwa elimu waliyopewa viongozi wa Serikali za mitaa na madiwani ni pamoja na maendeleo ya miradi mbalimbali ya umeme katika maeneo yao, elimu kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Umeme, pamoja na maboresho yanayoendelea katika eneo la huduma kwa mteja


.jpg)



EmoticonEmoticon