JENGO LA SHIRIKA LA BIMA YA TAIFA (NIC) KILIMANJARO LAWAKA MOTO.

January 23, 2014

JENGO la Shirika la Bima la Taifa, mkoani Kilimanjaro (NIC), juzi  lilinusurika kuteketea kwa moto baada ya moto mkubwa kuibuka katika  moja ya Vyumba vya ofisi zake na kuteketeza baadhi ya nyaraka muhimu kabla ya zima moto kufika na kuuzima kabla haujasababisha madhara  makubwa.


Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa mashuhuda wakiwemo baadhi ya  wafanyakazi wa shirika hilo, lililoko katika Jengo namba 2021, mtaa wa  TRA, Manispaa ya Moshi, mkoani hapa, moto huo ulianzia katika moja ya  vyumba vinavyotumika kuhifadhia nyaraka za Bima.
Baadhi ya maeneo ya ofisi katika Jengo hilo yaliyoathirika na moto huo
TAIFA LETU.com ilifika katika eneo la tukio na kukuta sehemu kubwa ya  moto huo ukiwa umeshazimwa kutokana na juhudi za pamoja ya wafanyakazi  wa Shirika hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha zimamoto, ambao tofauti ilivyozoeleka walifanikiwa kuwahi kufika  katika eneo la tukio.

Polisi wakikagua Baadhi ya maeneo ya ofisi katika Jengo hilo yaliyoathirika na moto huo

Akizungumza na gazeti hili kuhusu chanzo cha moto huo, Meneja wa  shirika hilo mkoani Kilimanjaro, John Mdenye alisema chanzo cha moto  huo haujafahamika bado na kuongeza kuwa alipata taarifa kutoka kwa katibu wake kuhusu kuonekana kwa Moshi ikitokea katika moja ya Stoo za  Shirika hilo.

Meneja wa NIC mkoani Kilimanjaro, John Mdenye akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu chanzo cha moto huo
“Nilikuwa Ofisini tangu saa mbili asubuhi, majira ya saa sita hivi,  Principle wangu alikuja na kunieleza kuwa kuna moshi katika stoo yetu  ya kuhifadhia faili za bima, baada ya kama dakika 10 kuliibuka moto mkubwa kutokea maeneo hayo, haraka niliwasiliana na zima moto ambao  walikuja kutoa msaada,” alisema Mdenye.

Mmoja wa Wafanyakazi akizungumza na Waaandishi wa Habari
Aidha Meneja huyo alisema mpaka sasa haijafamika moto huo utakuwa  umesababishwa na nini japo wanahisi huenda moto huo utakuwa umeanzia  katika ngazi za kupanda juu ambako kuna nyumba ya mpangaji mmoja  ambaye ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Gari la zimamoto likiondoka katika eneo la Jengo la Shirika la Bima ya Taifa, lililowaka moto
Alisema hisia hizo hata hivyo hazitoi uthibitisho wa moto kuanzia  katika nyumba ya mpangaji huyo kwani kilichoonekana mpaka sasa ni  kuwepo kwa mtungi wa gesi katika sehemu ya chini ya ngazi hizo hivyo kutoa wasiwasi huenda mpangaji huyo alikuwa anapikia hapo kutokana na sheria katika mkataba kutomruhusu kupika katika nyumba yake iliyoko  ghorofani kwa usalama wa ofisi za bima zilizoko chini.


 
Mpaka sasa haijafahamika kiasi cha thamani ya mali iliyoharibiwa  kutokana na moto huo japo hadi mwandishi wa gazeti hili anaondoka katika eneo la tukio, mali iliyoripotiwa kuharibika ni faili zote za bima zilizoteketea katika moto huo, kompyuta mbili moja ikiwa ni kompyuta mpakato ya Meneja huyo.

chanzo:www.kijiwechetu.blogspot.com 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »