WAZIRI NDEJEMBI AZUNGUMZA NA WATAALAMU WA IDARA MBILI NDANI YA WIZARA YA NISHATI

November 21, 2025




📌aweka msisitizo wa ukamilishaji wa vipaumbele ndani ya siku 100.


Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi, pamoja na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Salome Makamba, wameongoza kikao cha watumishi kutoka katika Idara mbili ndani ya Wizara ambazo ni Idara ya Umeme na Nishati Jadidifu pamoja na Idara ya Petroli, Jijini Dodoma. 


Mhe. Ndejembi ameeleza lengo la vikao hivi ni kutaka kujua wajibu tulio nao sisi kama Wizara ya Nishati, ndani ya siku mia moja, na njia sahihi tunazoweza  kuzitumia kufikia vipaumbele vya Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

“ Ni matamanio yangu sisi kama Wizara, ndani ya siku mia moja tuwe tumekamilisha vipaumbele hivi sawasawa na matamanio ya Mhe. Rais wetu ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi mbalimbali iliyopo ndani ya Wizara ya Nishati” amesema Mhe. Ndejembi.

Nae Kamishina wa umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga amesema, “Hali ya upatikanaji wa umeme nchini imeendelea kuimarika kutokana kukamilika kwa Mradi ya kuzalisha Umeme wa Kinyerezi I (MW 335), na Mradi wa ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (MW 2115) na kuongeza kuwa Umeme unaopatikana nchini kwa sasa ni jumla ya MW 4,383.74” amesema Mha. Luoga.

Aidha Mha. Luoga ameeleza kuwa mahitaji ya Umeme nchini yanakuwa kwa wastani kati ya asilimia 10 na 15, ambapo kwa sasa mahitaji hayo yamefikia wastani wa MW 2,450.73 ambapo mahitaji ya juu yaliyofikiwa katika Gridi ya Taifa hadi kufikia  Novemba 17, 2025 ni MW 2,044.53, na mahitaji ya juu kwenye maeneo yaliyo nje ya Gridi ya Taifa ni MW 406.2.

Mha. Luoga ameendelea kueleza kuwa Idadi ya wateja waliounganishwa umeme ni 5,689,557’ na Wananchi waliofikiwa na miundombinu ya umeme ( electricity access) ni asilimia 85.5 ambapo wateja wa Mjini ni 99.8% na wateja wa Vijijini ni 78.1%.

Kamishna Luoga  aliongeza kuwa wananchi waliounganishwa umeme (electricity connectivity) ni asimilia 52.1 ambapo wateja wa mjini ni 76.5% na wateja wa vijijini ni 37.1%, na Jumla ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vimeunganishwa Umeme, huku vitongoji 38,645 vimeshaunganishwa kati ya vitongoji 64,359 vya Tanzania Bara sawa na asilimia 60, vitongoji vilivyobaki ni 25,714 ambavyo vitaunganishwa umeme katika kipindi cha miaka mitano (2025-2030).

Nae Kamishina wa Petroli Bw. Godluck Shirima akitoa tathmini ya utekelezaji wa idara yake amesema,jumla ya visima 96 vyenye kina kirefu vimechimbwa kote nchini ambapo visima  ki 59 vipo nchi kavu na 37 vipo baharini. 


Kwa upande wa Gesi asilia Wizara imeandaa mpango mkakati wa gesi asilia (Natural gase Utilisation master plan - NGUMP) 2016-2045 , ikiwa ni mpango wa Serikali wa muda mrefu wa namna bora ya kutumia gesi asilia kwa maendeleo endelevu ndani ya nchi,huku ikitumika kusukuma jitihada za uendelezaji wa viwanda na kuhakikisha usalama nishati nchini. 

Shirima, amesema mkakati huu unatoa muongozo katika namna bora ya kutumia gesi asilia katika sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uzalishaji wa umeme, Viwanda, Usafirishaji wa matumizi wa gesi majumbani.


Mhe. Ndejembi amepongeza Idara zote mbili kwa kazi nzuri wanazo endelea kuzifanya lakini amesisitiza ukamilishaji wa Miradi kwa wakati ili kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu wa sita kufikia malengo yake ifikapo 2030. ili twende na dhamira ya dhati ya kuisaidia nchi yetu



Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Idara ya Umeme na Nishati Jadidifu pamoja na Idara ya Petrol ndani ya Wizara ya Nishati.


#NishatiTupokazini.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »