HALMASHAURI YA JIJI LA TANGA YAKUSUDIA KUTUMIA BILIONI 61.

January 30, 2014
                            Na Elizabeth Kilindi,Tanga.
                     
HALMASHAURI  ya  Jiji la Tanga imekusudia kutumia  zaidi ya tsh billion 61.1 kwa ajili  ya uendeshaji  wa  miradi mbalimbali ya  Jiji hilo  na utoaji wa huduma kwa wananchi katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015.
 
Hayo yalielezwa na meya wa Jiji la Tanga, Omari Gulled wakati akitoa taarifa kwa wananchi  kuhusiana na mchakato wa bajeti ya halmashauri hiyo na mipango  iliyopo  ya  uendeshaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi wake.
 
Gulled alisema kuwa bajeti hiyo imekamilika baada ya taratibu zote kufuatwa ikiwemo michakato ya kamati mbalimbali  na kwamba kamati hizo zimehitimisha kazi zake mapema ya January 11 ya mwaka huu.
 
Hata hivyo meya huyo alifafanua kuwa katika bajeti hiyo mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia tsh billion 7.7 ambapo tsh million 380  kati ya hizo ni ruzuku kutoka serikalini,wahisani na michango ya wananchi.
 
Alieleza kuwa tsh billion 13 ni fedha zinazotarajiwa  kupatikana  kwa kutokana na mradi  unaofadhiliwa na benk ya dunia kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo na huduma za kijamii.
 
“Miradi mikubwa tuliyonayo ni barabara,ujenzi wa kituo kipya cha mabasi  ya mikoani kinachojengwa Kange……..haya yote ni utekelezaji wa mwaka 2014/2015 kulingana na upatikanaji wa fedha tarajiwa” alisema Gulled.
 
Aidha aliitaja miradi midogo ya ndani inayotarajiwa kutekelezwa  katika Jiji hilo  kwa kipindi hicho kuwa ni ujenzi wa maabara kwa kila sekondari ya Kata, madawati, ukarabati wa barabara za Jiji, vituo vya afya, ujenzi wa hospitali ya Wilaya, mradi wa maji na umeme.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »