January 17, 2014

CCM TAIFA KUFANYA SHEREHE ZAKE ZA MIAKA 37 MKOANI MBEYA!!


 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godphrey Zambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki alisema sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika Februari 2, Mwaka huu.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza  Mwenyekiti wa CCMmkoa wa Mbeya
Charles Mwakipesile Mjumbe wa NEC
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godphrey Zambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki akiwa na katibu wa ccm mkoa wa Mbeya Maganga Sengerema

*******
RAISI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya Miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama hicho zitakazofanyika kitaifa Mkoani Mbeya.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari  katika Mkutano uliofanyika katika Ofisi za Chama hicho Mkoa zilizopo Sokomatola Jijini Mbeya, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godphrey Zambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki alisema sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika Februari 2, Mwaka huu.
Zambi alisema maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama cha mapinduzi ambayo yatafanyika kitaifa Mkoani Mbeya na Raisi Kikwete kuwa Mgeni rasmi yataanza majira ya saa 12 alfajiri kwa  kufanya matembezi ya Mshikamano.
Alisema matembezi hayo yataanzia katika viwanja vya John Mwakangale (nanenane) na kuishia katika Ofisi za Chama Mkoa eneo la Sokomatola yakihusisha Viongozi wa Chama na Wananchi mbali mbali wa Mkoa wa Mbeya na mikoa jirani.
Aliongeza kuwa baada ya matembezi hayo Wananchi na viongozi watapata mapumziko kidogo na kisha kuendelea na sherehe katika Viwanja vya Kumbu kumbu ya Sokoine zitakazoanza majira ya Saa nane Mchana.
Aidha mwenyekiti huyo alikipongeza Chama cha Mapinduzi Taifa kwa kuuteua Mkoa wa Mbeya kuwa Mwenyeji wa Sherehe hizo ambazo hazijawahi kufanyika Mkoani Mbeya tangu kuzaliwa kwa Chama hicho Mwaka 1977.
Alisema ni fursa pekee ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya ya kukutana na Raisi Kikwete ambaye ataweza kuwaeleza wananchi mafanikio yaliopatikana Mkoani Mbeya tangu kuzaliwa kwa Chama hicho hadi sasa.
Aliyataja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na Ongezeko la Vyuo vikuu ambavyo awali havikuwepo Mkoani Mbeya sambamba na kuimarishwa kwa miundombinu hususani ujenzi wa barabara za Lami ambazo Mbunge wa Chadema Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi anadai yeye ndiye amejenga.
Alisema mafanikio mengine wanayopaswa kujivunia wakazi wa Mkoa wa Mbeya ni pamoja na sekta ya Elimu, Afya, Maji na Umeme ambapo sehemu kubwa ya Mkoa wa Mbeya wenye wakazi zaidi ya Milioni Mbili na Wanachama wa chama hicho zaidi ya Laki tatu wakipata huduma bora za kijamii.
Zambi aliongeza kuwa kutokana na kufanyika kwa sherehe za maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM Mkoani Mbeya, Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho ambao awali ulitarajiwa pia kufanyika Mkoani hapa umeahirishwa na kuhamishiwa mkoa mwingine ambao haukutajwa.
Wakati huo huo Mwenyekiti huyo alizungumzia mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kwamba CCM haihusika nao kama baadhi ya watu wanavyodai.
Alisema Chama cha Mapinduzi hakifurahii migogoro ya vyama vya upinzani kwa sababu vilianzishwa kwa lengo la kuikumbusha Serikali iliyopo madarakani pindi inapofanya vibaya au kujisahau katika kufanya shughuli za kuwaletea Maendeleo Watanzania.
Alisema hata ndani ya CCM matatizo kama hayo hutokea lakini humalizwa kupitia vikao halali vya chama na kuendelea na shughuli zake kama kawaida na sio kukimbilia kwenye vyombo vya habari kutangaziana mabaya.

Na Mbeya yetu

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »