Na Oscar Assenga, Muheza.
MKUU wa
Mkoa wa Tanga, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa amewataka madereva mkoani Tanga
kuhakikisha wanajiepusha na ajali barabarani kwa kutoendesha mwendo kasi hasa katika kipindi hiki cha
sikukuu za mwishoni mwa mwaka.
Gallawa
alitoa kauli hiyo juzi wilayani hapa wakati akizungumza wananchi wa mkoa wa
Tanga mara baada ya makabidhiano ya zawadi za krismas zilizotolewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete katika makazi ya wazee
wasiojiweza misufini kata ya Ngomeni wilayani hapa.
Alisema
kuwa mara nyingi wakati wa sikukuu na mwishoni mwa mwaka madereva wengi
wamekuwa wakiendesha magari yao
kwa mwendo kasi bila kujali kuwa wanaweza kukumbana na ajali na kupoteza maisha
ya watu pamoja na kuleta simazi kwa Taifa.
“Nasisitiza madereva acheni kuendesha
magari mwendo kasi kwani bado tuna majonzi ya ajali zilizotokea ndani ya mwaka
huu na kusababisha maisha ya raia wasio na hatia kukatizwa huku wengine
wakibaki na ulemavu wa kudumu “Alisema Gallawa.
Katika
hatua nyengine, Gallawa aliwataka wananchi wa mkoa wa Tanga kudumisha utulivu
na amani kwa kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani na kuwa mstari wa
mbele kutoa taarifa kwa vyombo husika kwa viashiria vya kutoweka kwa amani.
Hata
hivyo mkuu wa mkoa huyo alisisitiza suala la usafi katika maeneo mbalimbali
jijini hapa kwa kuwataka wananchi kuendelea kuyaweka mazingira yao katika muonekano mzuri kwa wageni na
wenyeji.
Katika
makadbidhiano hayo, Mkuu huyi wa mkoa alikabidhi zawadi zilizotoka kwa Mh.Rais
mchele Kilo 150, mbuzi watatu(3),na mafuta ya chakula lita 40,miche mitano ya
sabuni pamoja na katoni moja ya chumvi vyote vikiwa na thamani ya fedha taslimu
sh.615,000.
Wakati
huo huo,Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limesema hakuna matukio matukio makubwa
yaliyojitokeza katika kusheherekea sikukuu ya krismas iliyoazimishwa jana
katika maeneo mbalimbali nchini.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga,Kamishna Msaidizi wa Polisi ,Constatine Massawe alisema
jeshi la polisi mkoani hapa limejipanga
vizuri katika kukabiliana na matukio yoyote ya kiuhalifu ambayo yanaweza
kujitokeza katika kipindi hiki cha sikukuu na mwisho wa mwaka.

EmoticonEmoticon