Imewekwa Desemba 27 saa 12:16 USIKU.
Wakazi
wa Jiji la Tanga wametahadharishwa kuwepo kwa mchafuko wa bahari, hali
inayotokana na kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya
Hindi na Visiwa vya Comoro.
Kufuatia hatua hiyo, wananchi
wote hususan wavuvi na waogeleaji baharini wanaagizwa kuchukua ahadhari
kubwa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.
Akizungumza katika mahojiano
na NIPASHE, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego, alisema kuwa kwa
mujibu wa taarifa walizozipata kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA), hali hiyo itapelekea bahari kuwa na mawimbi makubwa sambamba na
upepo mkali.
Dendego alisema kuwa
mabadiliko hayo ya hali ya hewa yanataraji kuukumba Mji wa Tanga kuanza
juzi jioni hadi Desemba 26 leo, hivyo wananchi wachukue tahadhari
kwenye maeneo ya Pwani.
“Tunajua kuwa starehe yetu
watu wa Tanga ni kutembea katika fukwe na wengine kuogelea. Vilevile,
shughuli za kiuchumi ikiwemo uvuvi hufanyika baharini hivyo natoa wito
kwa wananchi kuchukuwa tahadhari na kama inawezekana kutofika kabisa
kwenye maeneo hayo,” alisema.
Nao baadhi ya wavuvi
wakizungumza katika mahojiano na NIPASHE, walisema kuwa mpaka sasa wapo
baadhi ya wenzao ambao walienda baharini na hawajarudi na hawana uhakika
wa usalama wao kwani kumekuwa na mchafuko mkubwa wa bahari.
“Ni kweli kumekuwa na mchafuko
mkubwa sana wa bahari si unaliona wimbi hilo linavyovuma na kuna
wenzetu walienda baharini jana (juzi) hatujui hatma yao,” alisema
Mbaruku Jumaa.
Hata hivyo, walisema kuwa
wameshatoa taarifa kwenye mamlaka husika na kwamba hatua za ufuatiliaji
zimeanza kuchukuliwa ili kubaini iwapo kuna waliopata madhara kutokana
na machafuko hayo.
CHANZO: NIPASHE
EmoticonEmoticon