KIGOMBE BINGWA WA KOMBE LA MKONGE CUP 2013

December 06, 2013


Na Oscar Assenga,Tanga.

TIMU ya Shamba la Mkonge la Kigombe mkoani Tanga leo wameibuka na ubingwa wa Kombe la Mkonge Cup mara baada ya kuibamiza China Farm ya Morogoro mabao 4-3 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye dimba la soka Mkwakwani.



Katika mchezo ambao ulikuwa mkali na wenye upinzani mkubwa ambapo mpaka timu zote zinakwenda mapumziko hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzie,kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya mashambulizi kwa timu zote.



Wakionekana kujipanga na kujiimarisha vilivyo,Kigombe waliweza kufanya mashambulizi ya kushtukiza langoni mwa China Farm na kufanikiwa kuandika bao lao la kwanza dakika ya 56 kupitia Said Yasin kwa njia ya penati iliyotokana na mshambuliaji wa China Farm kumchezea faulu eneo la hatari Abdallah Maduba.




Kutokana na hali hiyo ilimlazimu mwamuzi wa mchezo huo,Ibrahimu Kidiwa “Mdudu”kuamuru ipigwe penati na ndipo ilipofungwa kiufundi na mchezaji huyo ambaye pia aliweza kutengeneza nafasi nyingi kwa timu hiyo.



Baada ya bao hilo,China Farm waliweza kujipanga na kuanza kufanya mashambulizi ya ,mara kwa mara langoni mwa Kigombe na kuweza kufanikiwa kusawadhisha bao hilo dakika ya 70 kupitia kwa Peter Bukulu ambaye aliweza kuunganisha krosi iliyopigwa na Rashid Paulo.



Mpaka dakika 90 zinamalizika timu hiyo zilitoka nguvu sawa na kuongezwa dakika 30 na mwamuzi wa mchezo huo ambazo hazikuweza kuzaa matunda yoyote ndipo ilipoamuliwa kupigwa mikwaju ya penati.



Katika hatua hiyo ya matuta ndipo timu ya Kigombe ilipoweza kuibuka na ushindi kwa kufanikiwa kufunga penati 4-3 dhidi ya wapinzani wao China Farm kitendo ambacho kilipelekea mashabiki wa timu hiyo kulipuka kwa shangwe na nderemo uwanja mzima.



Akizungumzia mashindano hayo,Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano,Lai Mpuma alisema mwaka huu yalionekana kuwa na msisimuko mkubwa iliyotokana na timu nyingi shiriki kufanya maandalizi kabambe na hivyo kupelekea kutokutabirika kuwa nani atachukua ubingwa.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »