WAZEE WAIOMBA SERIKALI KUWAONGEZEA FEDHA ZA PENSHENI

November 06, 2013


WAZEE wastaafu  ambao walikuwa watumishi wa Umma wameitaka Serikali kuwaongezea  fedha  za  Pensheni kutokana na kwamba  gharama za maisha zimepanda hivi sasa.

Sambamba na hilo pia wastaafu hao wapatao 5000 katika wilaya hiyo wameitaka Serikali kuwaeleza kwa nini wanacheleweshewa malipo yao ya pensheni hawapati  kwa wakati unaotakiwa.

Hayo yamesemwa na wastaafu hao katika kikao chao kilichofanyika katika ukumbi wa Bomani ambapo mgeni rasmi alikuwa Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) wilayani Muheza, Laick Gugu.

Akizungumzia kuhusu ongezeko la Pensheni Ibrahim Shemdoe amesema kuwa Serikali ilishatoa agizo kule hazina toka mwaka 2009 kwamba wastaafu waongezewe pensheni lakini mpaka sasa hawajapata kitu.

Shemdoe amesema kuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo pamoja na Rais Jakaya Kikwete walishatoa agizo wastaafu hao waongezewe pensheni lakini maagizo yao yamedharauliwa.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika mkutano huo, Gugu amesema kuwa kama wataanzisha umoja huo wa wazee wastaafu basi waanzishe Chama cha kuweka na kukopa (SACCOS) na atawachangia sh.milioni 1 ya kufungua akaunti huku akisema pia itakuwa rahisi kuchangiwa na watu wengine.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »