MAKANGALE STAR NA VUMAWIMBI BOYS WAMELIZA TOFAUTI ZAO.

September 09, 2013
Na Masanja Mabula -Pemba .
Mahasimu wa soka katika Wilaya ya Micheweni Timu ya Makangale Star na Vumawimbi Boys wameondoa tofauti zao na kuamua kuunganisha timu lengo ni kupata timu moja yenye nguvu na ambayo italeta ushindani kwenye michuano ya ligi daraja la pili Wilayani humo .

Taarifa ambazo zimepatikana kutoka kwa moja wa viongozi wa Timu hizo zenye maskani yake katika Shehia ya Makangale,   zinasema kwamba tayari makubaliano ya kuunganisha timu hizo yamefikiwa na kupewa baraka na chama cha soka Wilaya ya Micheweni .

Msemaji wa Klabu ya Makangale Star Rashid Ali Juma Sendeu amesema kuwa katika makubaliano hayo kila timu imetakiwa kutoa wachezaji kumi na tano ili kufanya idadi ya wachezaji thelesini wanaotakiwa kwenye fomu ya usajili .

Aidha amefahamisha kwamba timu ambayo imepatikana kutokana na muungano huo umesajiliwa kwa jina la Makangale United na inatarajia kushiriki ligi daraja la pili Wilaya hiyo na kwamba kwa sasa inaendelea na mazoezi katika kiwanja wa Skuli ya Makangale .

Na katika kuimarisha na kuleta mafaniko ya klabu , tayari umeundwa uongozi pamoja na kuanzisha kamati mbali mbali ambazo zitakuwa na jukumu la kusimamia maendeleo ya klabu hiyo .

Waliochaguliwa kuunda kamati hizo ni wazee wawili kutoka kila timu huku aliyekuwa kocha wa Klabu ya Makangale Star Juma Mbirimbi amepewa jukumu la kuinoa klabu hiyo akisaidiwa na Ali Mussa .

Mmoja wa washambuliaji wa kutegemewa wa klabu hiyo Mussa Ali Baby akizungumza na mwandishi wa habari hizi amekiri kuwepo na ushindani wa namba na kusema itakuwa vigumu mchezaji kujihakikishia namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza .

Hata hivyo mpachika mabao huyo ameahidi kutumia uwezo na kujituma ili aweze kumshawishi kocha ili aweze kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza licha ya kwamba timu imesajili wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa .

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »