KONDE STAR NA MAENDELEO MANTA KUPAMBANA IJUMAA LIGI DARAJA LA KWANZA PEMBA.

September 19, 2013
Na MASANJA MABULA -PEMBA.
Timu mbili zenye upinzani mkubwa kutoka Jimbo la Konde  na ambazo zinashiriki ligi daraja la kwanza Taifa Pemba , Konde Star na Maendeleo Manta zitapambana  katika uwanja wa Kinyasini Ijumaa ya 20 kutafuta nafasi ya kucheza ligi kuu ya Zanzibar kwa msimu ujao .

Timu hizo ambazo zote inaaminika kwamba zinadhaminiwa na Wabunge , Yussuf Salim Hussein Kibiriti  wa Jimbo la Chambani ( Maendeleo Manta ) na Khatib Said Oboma wa Jimbo la Konde (  Konde Star) zinatarajia kutoa burdani na kuufanya mchezo huo kuwa na ushindani wa hali ya juu .

Katika mchezo huo ambao mashabiki wa Mpira katika Jimbo la Konde na Wilaya ya Micheweni wameanza kutabiri na kusema kuwa itakuwa ni vita kati ya Obama na Kibiriti ambao kwa pamoja wameonesha nia ya kutaka kuinua kiwango cha soka Jimboni humo .

Tayari katika michezo yake ya awali , viongozi hao waliziongoza timu zao kufanya mauwaji , kwa timu ya Maendeleo Manta kuifunga timu ya Opec  ya Pandani bao 1-0 ambapo mbunge huyo aliahidi kutoa kitita cha shilingi milioni moja baada ya timu hiyo kuifunga Opec .

Naye Obama alihudhuria kwenye mchezo uliofanyika katika uwanja wa Ngerengere jeshini , na kushuhudia timu ya Konde Star ikitoa kipigo cha paka mwizi kwa timu ya Coast Ilanders ya  kutoka Wilaya ya Mkoani cha mabao 4-0.

Kwa matokeo hayo , kila upande umetamba kuondoka na ushindi katika mchezo huo ambao pia umeteka nyoyo z awapenda soka Kisiwani Pemba .

Katika msimu uliopita timu zilikutana mara mbili ambapo katika mchezo wa awali Maendeleo Manta walishinda kwa jumla ya mabao 3-2 ambapo katika mchezo wa marudiano Konde Star iliishinda kwa jumla ya mabao 3-1 michezo yote ilichezwa katika uwanja wa Gombani .


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »