Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Mechi tano kati ya sita za Super Week za Ligi Kuu ya
Vodacom zilizokuwa zioneshwe moja kwa moja (live) na Kituo cha televisheni cha
SuperSport cha Afrika Kusini sasa hazitaoneshwa kutokana na matatizo ya
kiufundi.
Kwa mujibu wa Mtayarishaji Mtendaji (Executive Producer)
wa SuperSport Kanda ya Afrika, Max Tshunungwa ambaye yuko nchini, wameshindwa
kuonesha mechi hizo kutokana na matatizo ya kiufundi katika magari yao ya
kurushia matangazo (OB van) yanayohudumia Afrika Mashariki- Kenya, Tanzania na
Uganda.
Mechi hizo ni kati ya Azam na African Lyon, Yanga na
Oljoro JKT, Azam na Simba, Coastal Union na JKT Ruvu na Mgambo Shooting na Yanga
itakayochezwa Aprili 17 mwaka huu jijini Tanga.
Tatizo hilo pia limeathiri mechi za Ligi Kuu ya Kenya
(KPL) ambazo hazitaonekana wikiendi hii. SuperSport ndiyo yenye haki za
matangazo ya televisheni kwa ligi hiyo ya Kenya.
Tshunungwa amekutana na Sekretarieti ya TFF na Kamati ya
Ligi kuelezea tatizo hilo. SuperSport kwa kushirikiana na Kamati ya Ligi na TFF
watapanga mechi nyingine za Super Week kabla ya ligi kumalizika msimu
huu.
Pia TFF, Kamati ya
Ligi na SuperSport watakuwa na mkutano mfupi wa waandishi wa habari wakati wa
mapumziko kwenye mechi ya leo kati ya Yanga na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa
Taifa.
MWISHO.
EmoticonEmoticon