Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kushoto)
akijadiliana jambo na Kamishna wa Nishati, Mhandisi Hosea Mbise
(katikati). Wa kwanza kulia ni Kamishna Msaidizi anayeshughulikia
Maendeleo ya Nishati, James Andilile.
Wajumbe wa kikao wakimsikiliza katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo.
Mkurugenzi
Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi (kushoto) akizungumza wakati wa kikao
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo
(kulia). Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi- EWURA, Profesa
Jamidu Katima.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kulia)
akipokea nyaraka mbalimbali kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi- EWURA, Profesa Jamidu Katima. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi
Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi.
Taasisi
zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini zimeagizwa kutochelewesha
kushughulikia maombi ya wawekezaji pale wadau mbalimbali wa ndani na nje
ya nchi wanapoonesha dhamira ya kuwekeza. Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo ametoa agizo hilo hivi karibuni
wakati wa kikao chake na Watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA) pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo.
Mhandisi
Chambo aliwaagiza watendaji hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea, na
badala yake wazingatie Sheria na maadili ya kazi zao, kutokana na ukweli
kwamba sekta ya Nishati ni sekta nyeti inayohitaji watendaji waadilifu
na wabunifu.
“Akitokea
mwekezaji ambaye ameonesha nia ni vema ajibiwe haraka bila kuchelewa
iwe amekubaliwa au kukataliwa ombi lake; hakuna sababu ya kumzungusha
mwekezaji; tuzidishe kasi ya uwajibikaji,” alisema Mhandisi Chambo.
Alisema
lengo la Serikali ni kuongeza uwekezaji hususan kwenye sekta za Nishati
na Madini na hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha uwekezaji kwani fursa
za uwekezaji zilizopo nchini ni nyingi.
Aliwaasa
EWURA na Taasisi nyingine kuacha tabia ya woga, na kusema kwamba endapo
itatokea mwekezaji akatuma maombi ya kuwekeza nchini, wanapaswa kupitia
maombi husika, kujiridhisha na kutoa maamuzi kwa haraka na kwa
kujiamini.
“Tufikie
mahali tufanye maamuzi. Msiwe na woga kwenye kutekeleza jambo lenye
maslahi mapana ya Kitaifa; majibu ya njoo kesho hatutayavumilia,”
alisema.
Vilevile
Mhandisi Chambo alisema ni vyema taasisi zilizo chini ya Wizara ya
Nishati na Madini zikashirikiana na Wizara katika kufanya upembuzi
yakinifu wa miradi katika maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji. Aidha,
aliwaagiza watendaji kukaa pamoja kujadili maeneo ya kipaumbele ili
upembuzi yakinifu ufanyike kwa lengo la kurahisisha majadiliano na
wawekezaji.
Alisema
ni vyema ikaundwa timu ya wataalamu kutoka katika Taasisi na Wizara
ambao watahusika moja kwa moja na suala la kubaini maeneo pamoja na
kufanya upembuzi yakinifu kwa miradi yenye tija na manufaa na hivyo
kufikia mwafaka mapema na kuanza utekelezaji wa mradi husika pale
mwekezaji anapojitokeza.
“Ikitokea
mwekezaji akaonesha dhamira ya kuwekeza kwenye maeneo husika ni vema
taarifa za awali zikawepo. Hii itavutia wawekezaji wengi zaidi lakini
pia itaharakisha majadiliano,” alisema. Aidha, Mhandisi Chambo
aliwapongeza EWURA kwa kufanya vizuri kwenye masuala ya mafuta na
kuwaasa kujitahidi kufanya vizuri katika majukumu mengine yaliyo chini
yao. Naye Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi aliahidi kufanya
kazi kwa uadilifu na kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu
pamoja na kumpatia ushirikiano wa kutosha. Kikao hicho ni mwendelezo wa
vikao vya Katibu Mkuu huyo na Menejimenti pamoja na Bodi za Taasisi
zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ili kupata ufumbuzi wa
changamoto zinazozikabili.
EmoticonEmoticon