REA YAHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA WAJASIRIAMALI SONGWE
habariTANZANIA,BURUNDI ZAZINDUA UJENZI WA RELI YA SGR UVINZA- MUSONGATI
habari*_Kugharimu dola za Marekani bilioni 2.154_*
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo (Jumamosi, Agosti 16, 2025) ameshiriki uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa ya kutoka Uvinza hadi Musongati na kuwahahikishia Watanzania na WanaBurundi kwamba ujenzi huo utaanza katika muda uliopangwa.
Waziri Mkuu ambaye ameshiriki hafla hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema reli hiyo itakayokuwa na urefu wa km.240 pindi ikikamilika, itakuwa ndiyo reli ya kwanza inayounganisha nchi na nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika eneo la Musongati, Burundi, Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo kutasaidia kuunganisha masoko na kuendeleza biashara baina ya Tanzania na Burundi.
"Reli ikikamilika itafungua fursa kwa wananchi wetu ambao wataweza kutoka hapa hadi Dar es Salaam ndani ya siku moja. Hata kwenye usafirishaji wa mizigo, hivi sasa, lori linatumia saa 96 kutoka Dar hadi Bujumbura lakini baada ya kukamilisha ujenzi, usafirishaji wa mizigo kwa kutumia treni utatumia saa 20 tu."
"Mradi wa reli ya kisasa siyo tu kwamba utarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, bali pia utafungua milango ya fursa mpya za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Burundi."
Akielezea kuhusu mradi huo, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa reli hiyo utagharimu dola za Marekani bilioni 2.154 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitano na kwamba mwaka mmoja baada ya ujenzi utakuwa ni wa matazamio.
Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Meja Jenerali Evarist Ndayishimiye alisema kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo kutatibu shauku ya muda mrefu ya nchi hiyo kuwa na usafiri wa reli.
"Leo ni siku ya furaha sana kwetu. Tumepata jawabu la tangu enzi na enzi. Mwaka 1921, mradi huu ulianzishwa na Wabelgiji kisha wakaja Wajerumani lakini wakashindwa. Leo hii Tanzania na Burundi tumeweza," alisema.
Alisema nchi yake imebarikiwa kuwa madini mengi na kuna wakati aliitisha kikao cha wawekezaji kutoka nchi kadhaa. "Wengi walivutiwa na wakataka kuwekeza mara moja, lakini wakaniuliza, tukianza kuchimba madini ya Nickel, tutayasafirishaje?"
"Hiyo changamoto ilitufanya tubungue bongo zetu na kutafuta suluhisho. Tunaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kukubali kuungana nasi ili tuanze mradi huu muhimu. Tukitoka hapa, tunataka reli iunganishe hadi Kindu, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Na baada ya hapo, tunataka reli yetu ifike Afrika Magharibi kwenye ufukwe wa bahari ya Atlantiki kwani tunaamini njia hiyo itaharakisha kuleta maendeleo."
Rais Ndayishimiye alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa kufikia hatua kubwa za maendeleo. "Ukirudi nyumbani mwambie Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba tunampongeza sana kwa kuleta maendeleo ya haraka nchini Tanzania."
"Nimekaa Tanzania kwa muda mrefu lakini kwa sasa nikija naweza kupotea. Magomeni napajua, Tabata na Vingunguti napajua, Mwenge napajua, na Kinondoni nilishakaa; lakini kwa sababu ya maendeleo yaliyopatikana, naweza kupotea. Tunamshukuru kwa uongozi wake imara,"
Rais huyo alizungumza kwa Kiswahili na kuamsha shangwe miongoni mwa wananchi waliohudhuria tukio hilo.
Mapema, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na Ajenda 63 ya Umoja wa Afrika ambayo inataka bara la Afrika liunganishwe kwa mtandao wa reli ya kisasa.
Alisema mbali na kuziunganisha nchi hizo mbili, kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo, kutarahisisha kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo. "Hivi sasa, kontena moja la futi 20 linasafirishwa kwa gharama ya dola za Marekani 3,800 lakini reli ikikamilika, gharama itashuka hadi dola za Marekani 2,000.
Alisema faida nyingine itakayopatikana baada ya mradi huo kukamilika ni kuwezesha kusafirisha mizigo mingi kwa wakati mmoja. "Hivi sasa, mzigo unaosafirishwa kwa lori moja ni tani 30, lakini reli ikianza kazi, tutaweza kusafirisha tani 3,000 kwa wakati mmoja," alisema Waziri Mbarawa.
(Mwisho)
Imetolewa na
Ofisi ya Waziri Mkuu,
Jumamosi, Agosti 16, 2025
WAANDISHI WA HABARI DODOMA WAPATIWA MAFUNZO YA USALAMA NA ULINZI
habariBaadhi ya waandishi wa habari kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (Dodoma Press Club) wamepatiwa mafunzo ya usalama wa kimwili, kidijitali na afya ya akili, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujilinda binafsi katika mazingira ya kazi.
Mafunzo hayo yalifanyika Agosti 16, 2025, yakiongozwa na Mkufunzi wa Usalama na Ulinzi, Okuly Julius, ambaye pia ni mwandishi wa habari. Okuly alipata mafunzo hayo kupitia Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kisha kupewa jukumu la kuwajengea uwezo waandishi wenzake katika mikoa.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Okuly amesema waandishi wa habari wanapaswa kuwa makini na kuchukua tahadhari muda wote kwani usalama huanzia kwa mwandishi mwenyewe.
“Ni muhimu kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya mashambulizi ya kimtandao kwa kuhakikisha viunganishi vinavyopokelewa vinathibitishwa kabla ya kubofya, kutumia nywila imara na kuweka uthibitishaji wa hatua mbili. Waandishi wanapaswa kuwa makini zaidi hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, kipindi ambacho mara nyingi huambatana na vitisho, ukatili na hata kukamatwa kiholela,” alisema Okuly.
Ameongeza kuwa ni vyema waandishi kutoa taarifa kwa watu wa karibu au wenzao wanapokwenda kwenye kazi, ili kuepuka hatari zinazoweza kutokea endapo watapatwa na matatizo wakiwa peke yao.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Bahati Msanjila (Crown Media), Saida Issa (Gazeti la Zanzibar Leo), Rhoda Simba (Channel Ten), Gideon Gregory (Jambo FM) na Joyce Kasiki (Gazeti la Majira), walisema yamewajengea uwezo mkubwa na sasa wanafahamu mbinu bora za kufanya kazi kwa usalama.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa “Empowering Journalists for Informed Community” (Kuwawezesha Waandishi wa Habari ili Jamii Iweze Kupata Taarifa Sahihi) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC). Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa International Media Support (IMS), Union of Tanzania Press Clubs (UTPC) na JamiiAfrica.
TUKITUMIA NISHATI SAFI YA KUPITIKIA TUTAOKOA HEKTA 400,000 ZA MISITU ZINAZOTEKETEA KWA MWAKA -MJIOLOJIA NSAJIGWA
habari📌 *Awanoa Wanawawake na Wajasiriamali Songwe kuhusu Nishati Safi ya Kupikia*
📌 *Atoa wito kwa Wadau kushirikiana na Wizara ya Nishati kutoa elimu ya Nishati Safi ya Kupikia*
Songwe
Imeelezwa kuwa matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia si tu yanahatarisha afya bali pia yanachochea uharibifu wa mazingira ambapo takribani hekta 400,000 za misitu hupotea kila mwaka nchini kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa, jambo linalochangia kuongezeka kwa ukame na mabadiliko ya tabianchi.
Hivyo, Watanzania wameaswa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi kama kuni na mkaa kutokana na athari zake kwa binadamu na mazingira.
Wito huo umetolewa leo Agosti 16, 2025, na Mjiolojia kutoka Wizara ya Nishati, Nsajigwa Maclean, wakati akitoa elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Wajasiriamali mkoani Songwe.
Amesema kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, ni asilimia 16 tu ya Watanzania ndio wanaotumia nishati safi ya kupikia, hivyo bado kuna magonjwa yanayotokana na moshi wa kuni na mkaa, ambayo yanasababisha vifo vya zaidi ya watu 33,000 kwa mwaka nchini.
Katika ngazi ya kimataifa, amesema watu bilioni 2.1 hawana upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, huku zaidi ya watu milioni 3 wakifariki dunia kila mwaka kutokana na madhara ya kiafya yanayotokana na nishati isiyo safi ya kupikia ambapo Kusini mwa Jangwa la Sahara zaidi ya watu milioni 960 hawana nishati hiyo.
Aidha amebainisha kuwa kuna dhana potofu miongoni mwa jamii kuwa chakula kinachopikwa kwa kutumia gesi au umeme hakiwi na ladha nzuri, jambo ambalo amesema halina msingi wa kisayansi na linaendelea kuwazuia wananchi wengi kufanya mabadiliko kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Ameeleza kuwa Wizara ya Nishati imeweka mkakati wa kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, huku mkakati huo ukiangazia mafanikio kutoka nchi nyingine kama India na Ghana, ambazo zimepiga hatua katika kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Imeelezwa pia kuwa changamoto kubwa kwa wananchi si kutotaka kutumia nishati safi ya kupikia bali wanahitaji elimu pia kuhusu matumizi ya nishati hiyo hivyo ametoa wito kwa Wadau kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia.
Katika semina hiyo wanawake na wajasiriamali walihimizwa kuwa mabalozi wa mabadiliko kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia si kwa ajili ya afya pekee, bali pia kwa ajili ya kulinda mazingira na kizazi kijacho.