
✅Katika harambee hiyo Wadau na Waumini wamechangia Milioni 103
Na: OWM (KAM) – Dar es Salaam
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Evaline Munisi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuthamini mchango wa taasisi za dini katika kudumisha amani na kuchochea maendeleo ya jamii.
Dkt. Munisi amesema hayo leo Novemba 29, 2026 wakati akizungumza katika harambee ya kuchangisha Shilingi milioni 900 kwa ajili ya maendeleo ya jamii iliyofanyika katika Kanisa la TAG Kijichi Kati, Jimbo la Kigamboni, alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema taasisi za dini zina dhamana muhimu ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani. Alieleza kuwa viongozi wa dini wamekuwa mstari wa mbele kuelimisha waumini na jamii kupitia madhabahu na mimbari zao kuhusu umuhimu wa kudumisha amani, wakitambua kuwa bila amani shughuli za kijamii na za kidini haziwezi kuendelea.
Aidha, aliwapongeza viongozi wa dini kwa nafasi yao katika kuimarisha maadili, mshikamano wa kitaifa na ustawi wa jamii, hususan kupitia elimu wanayoitoa kwa vijana. Alisema mchango huo ni muhimu katika kujenga jamii yenye maadili na kuendeleza amani nchini.
Vilevile, amepongeza dhamira ya kanisa hilo ya kuelekeza sehemu kubwa ya fedha zitakazokusanywa katika harambee hiyo kutumika katika huduma za jamii, elimu, malezi na uwezeshaji wa wananchi, akisema hatua hiyo ni mfano wa namna taasisi za dini zinavyoweza kuwa washirika muhimu wa maendeleo.
Kadhalika, amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kulinda amani na utulivu nchini, akisisitiza kuwa milango ya ushirikiano ipo wazi kwa ajili ya kuimarisha mahusiano baina ya Serikali na taasisi hizo kwa ustawi wa jamii.
Naye, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke, Bi. Bertha Minga amesema kuwa wilaya hiyo imeendelea kuimarisha mahusiano na Taasisi za Dini pamoja na kushirikiana nazo katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la TAG Kijichi Kati, Jimbo la Kigamboni, amemshukuru Naibu Waziri Dkt. Munisi kwa kuendesha zoezi hilo la harambee na kueleza kuwa fedha hizo zitatumika kwa shughuli na huduma zilizopangwa katika kusaidia jamii.
“Katika hafla hii, fedha zitakazokusanywa zilipangwa kuelekezwa katika ujenzi wa madarasa na ofisi, kituo cha watoto yatima, pamoja na kuwasaidia wajane na watu wenye uhitaji” amesema
Awali akiwasilisha risala, Katibu wa Kanisa hilo Bi. Neema Maluka amesema kanisa hilo linaendelea kukua na kuwa chombo muhimu cha maendeleo ya kiroho na kijamii katika eneo la Kigamboni na jijini Dar es Salaam kwa ujumla, hivyo amehamasisha wadau kujitokeza katika kufanikisha harambee hiyo.

















EmoticonEmoticon