TBS YAPIGA KAMBI YA VIWANGO CLINIC JIJINI MWANZA

October 21, 2026
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesogeza huduma karibu na wananchi jijini Mwanza kupitia kambi maalum ya Viwango Clinic, ili kufikisha elimu kuhusu ubora wa bidhaa mbalimbali za chakula na vipodozi.

Kambi hiyo ya siku tano imeanza Jumatatu Oktoba 19, 2026 hadi Ijumaa Oktoba 23, 2025 inafanyika katika eneo la Soko Kuu jijini Mwanza, ikilenga pia kutoa elimu ya usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi.

Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, Happy Brown amesema kupitia kambi hiyo, wananchi na wafanyabiashara wamepata elimu na huduma mbalimbali kama vile uthibitishaji ubora wa bidhaa zinazozalishwa ndani na nje ya nchi.

“Tumesogeza huduma karibu kwa sababu eneo hili lina wafanyabiashara wengi ambapo katika kliniki hii tunatoa pia huduma ya usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi, usajili wa maduka, stoo na magari yanayosambaza bidhaa hizo” amesema Brown.

Ameongeza kuwa matarajio ya TBS ni kuona kliniki hiyo ikiongeza tija kwa wafanyabiashara na wananchi ambao kupitia elimu hiyo wataweza kutambua bidhaa zenye ubora na hivyo kuepuka madhara ya kutumia bidhaa zisizo na ubora na ambazo hazijasajiliwa.

Brown pia ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi na wafanyabiashara jijini Mwanza, kufika katika kliniki hiyo kupata elimu na huduma mbalimbali ikiwemo jinsi ya kupata vibali na nembo ya ubora wa TBS katika bidhaa wanazozalisha.

Nao baadhi ya wananchi wakiwemo wafanyabiashara wa bidhaa za chakula na vipodozi jijini Mwanza, wamesema kliniki hiyo imewasaidia kupata huduma papo kwa hapo na hivyo kuepuka adha ya kutumia muda mrefu kwenda ofisini. 

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »