UBUNIFU WA TANGA UWASA WAWAVUTIA HAZINA,MAMALAKA ZATAKIWA ZIIGE

October 06, 2026


Na Oscar Assenga,TANGA

MSAJILI wa Hazina Nehemiah Mchechu amezitaka mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira nchini kutumia ubunifu wa kutafuta fedha nje ya Serikali, ikiwamo kupitia sekta binafsi na jamii, ili kugharimia miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali.

Alitoa wito huo  wakati wa ziara ya kutembelea Mradi wa Kuboresha Hali ya Upatikanaji wa Maji Tanga Awamu ya Tatu, unaotekelezwa kwa fedha zilizopatikana kupitia Hatifungani ya Kijani yenye thamani ya Sh53.12 bilioni.

Mchechu amesema hatua iliyochukuliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) inapaswa kuwa mfano kwa mamlaka nyingine za maji nchini katika kutafuta fedha za kutekeleza miradi mikubwa.


Alisema wanaiangalia Tanga UWASA kwa wivu mkubwa kutokana na jinsi inavyofanya vizuri hiyo wanataka na taasisi zote za maji kuiga mfano wa Tanga Uwasa

Tanga UWASA imekuwa taasisi ya kwanza ya maji nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki kufanikiwa kupata na kuorodhesha Hatifungani ya Kijani kwa ajili ya kugharimia miradi ya majisafi, majitaka na uhifadhi wa mazingira.

Kwa Mchechu, hatua hiyo inaonyesha kuwa taasisi za umma zinaweza kutumia ubunifu kupata fedha za miradi bila kutegemea Serikali Kuu pekee.

Amesema iwapo mamlaka nyingine zitatumia mfumo huo, Serikali inaweza kupata nafasi ya kuelekeza fedha ambazo zingetumika kwenye miradi ya maji katika maeneo mengine ya kipaumbele cha maendeleo.

Mchechu, aliyeambatana na Menejimenti ya OTR, amempongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Tanga UWASA, Dk Fungo Fungo, pamoja na menejimenti ya mamlaka hiyo kwa ubunifu huo.

Amesema Tanga UWASA ni miongoni mwa taasisi 308 zinazopata usimamizi wa Hazina.

Wakati huo huo, utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya Sh53.12 bilioni umefikia asilimia 80.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga UWASA, Mha Salum Ngumbi, amesema mradi huo ulianza Oktoba 12, 2024 na unatarajiwa kukamilika Novemba 30, 2026.

Amesema ukikamilika, mradi huo utasaidia kuboresha huduma ya maji kwa wakazi takribani 600,000 wa Jiji la Tanga pamoja na miji ya Muheza na Pangani.
Mabayani kuongeza uwezo

Ngumbi amesema mradi huo unahusisha upanuzi wa Kituo cha Kusukuma Maji cha Mabayani, ambacho uwezo wake utaongezwa kutoka mita za ujazo 42,000 hadi 72,000 kwa siku.

Amesema kazi hiyo itahusisha ufungaji wa mashine nne za kusukuma maji, kila moja ikiwa na uwezo wa kusukuma mita za ujazo 1,500 kwa saa.

Pia, bomba kubwa lenye kipenyo cha milimita 600 linawekwa kutoka Mabayani hadi Mowe kwa urefu wa kilomita 6.4.
Mowe kuongeza uzalishaji

Ngumbi amesema Mtambo wa Kutibu Maji wa Mowe unapanuliwa ili kuongeza uwezo wa kutibu na kuzalisha maji kutoka mita za ujazo 45,000 hadi 60,000 kwa siku.

Aidha, mradi huo unahusisha upanuzi wa mtandao wa usambazaji maji kwa kilomita 60 pamoja na ununuzi na ufungaji wa mita 10,000 za maji za malipo kabla.

Amesema mita hizo zitasaidia kudhibiti upotevu wa maji na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

Majitaka, Mto Zigi vyapewa kipaumbele

Katika eneo la majitaka, Ngumbi amesema mradi huo unahusisha uendelezaji wa mtandao kwa urefu wa kilomita 1.5 na ukarabati wa bomba la majitaka lenye urefu wa kilomita tatu katika eneo la Ngamiani.

Amesema pia kuna shughuli za uhifadhi wa mazingira zinazolenga kuhakikisha uendelevu wa Mto Zigi.

Mradi huo, pamoja na kuongeza uwezo wa uzalishaji na usambazaji wa maji, unalenga kuboresha huduma za majitaka na kupunguza upotevu wa maji, hatua ambayo Tanga UWASA inatarajia kuongeza ufanisi wa huduma na mapato ya mamlaka hiyo.




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »