WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, akizungumza katika Mkutano wa Kwanza wa Wakurugenzi na Wasimamizi wa Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini uliofanyika leo Septemba 21, 2026, jijini Arusha.
***************
Na OWM (KAM), Arusha
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema Vitengo vya ufuatiliaji na tathmini vinawajibu wa kuisaidia serikali kufanya maamuzi sahihi, kuboresha utekelezaji wa mipango na kuhakikisha matumizi ya rasilimali za umma yanaleta matokeo chanya kwa wananchi.
Akifungua Mkutano wa Kwanza wa Wakurugenzi na Wasimamizi wa Vitengo hivyo leo Septemba 21, 2026, jijini Arusha, Mhe. Sangu amesema wataalamu wa vitengo hivyo wana jukumu la kuhakikisha mipango ya Serikali inatafsiriwa kuwa matokeo halisi yanayoboresha maisha ya wananchi.
“Wataalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini, ninyi ndiyo macho, pua na masikio mnaojenga mfumo wa Serikali wa kujua kama mipango tunayoiweka kwenye karatasi inabadilika kuwa matokeo halisi na kuleta tabasamu kwa wananchi,” amesema Mhe. Sangu.
Amesema kuanzishwa kwa vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini katika wizara, idara zinazojitegemea, wakala, mashirika ya umma, tawala za mikoa na serikali za mitaa ni hatua muhimu inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uwajibikaji na kupima matokeo ya utekelezaji wa mipango yake.
Aidha, amesema Serikali imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini kupitia Mfumo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini Serikalini (Government-Wide M&E System) pamoja na mifumo mingine ya kidijitali ikiwamo e-Delivery, hivyo kuwataka wataalamu kutumia kikamilifu fursa hizo katika kutekeleza majukumu yao.
Mhe. Sangu amewataka Wakurugenzi na wasimamizi wa vitengo hivyo kuzingatia uadilifu, uzalendo, ubunifu na ushirikiano, huku wakiwa na ujasiri wa kutoa taarifa sahihi zinazotokana na takwimu na ushahidi halisi ili kusaidia Serikali kufanya maamuzi kwa wakati.
“Tunapoelekea kwenye utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, tunapaswa kuwa na Ufuatiliaji na Tathmini wa kimkakati unaolenga matokeo na kutoa tahadhari mapema ili kuwezesha ufanyaji wa maamuzi stahiki na kwa wakati stahiki,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. James Kilabuko, amesema mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo Jumuishi wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini, unaolenga kuwakutanisha wataalamu ili kubadilishana uzoefu na kutathmini utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema hatua hiyo inalenga kujenga Taifa lenye uwezo wa kujifunza kutokana na matokeo ya shughuli za ufuatiliaji na tathmini na kutumia maarifa hayo kuboresha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Mkutano huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Kongamano la Tano la Kitaifa la Ufuatiliaji na Tathmini (Monitoring, Evaluation and Learning Week), linalotarajiwa kufanyika Septemba 22 hadi 26, 2026.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, akizungumza katika Mkutano wa Kwanza wa Wakurugenzi na Wasimamizi wa Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini uliofanyika leo Septemba 21, 2026, jijini Arusha.
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Kwanza wa Wakurugenzi na Wasimamizi wa Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, uliofanyika katika hoteli ya Ngurdoto Mountain leo Septemba 21, 2026, jijini Arusha.











EmoticonEmoticon