Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imewaalika waajiri na wamiliki wa viwanda nchini kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo katika kuandaa na kuendeleza wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alitoa kauli hiyo jana jijini Dodoma wakati wa hafla ya kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya VETA na Kampuni ya Van Mo, inayolenga kuimarisha ushirikiano katika kuwaendeleza vijana wenye ujuzi na kuwawezesha kupata ajira mara baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa katika Ukumbi wa Mikutano wa VETA Makao Makuu yalihusisha CPA Kasore kwa upande wa VETA na Meneja Mkuu wa Van Mo, Fathi Ahmed Ally. Kampuni hiyo inajihusisha na shughuli mbalimbali zikiwemo usafirishaji, uchukuzi, uuzaji wa mafuta, umiliki wa majengo na ardhi, kilimo, utalii pamoja na shughuli za uzalishaji viwandani.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, pande hizo zinalenga kuongeza upatikanaji wa wahitimu wenye umahiri, tija, ubunifu, maadili na wanaozingatia usalama kazini, huku Van Mo ikitoa fursa za ajira kwa wahitimu wa VETA wenye sifa zinazohitajika.
Aidha, ushirikiano huo utasaidia kuoanisha programu za mafunzo ya ufundi stadi na mahitaji halisi ya sekta ya viwanda na biashara pamoja na kuwawezesha wanafunzi kupata mafunzo kwa vitendo katika maeneo ya kazi.
Maeneo ya ushirikiano yaliyoainishwa katika MoU hiyo ni pamoja na mafunzo ya udereva wa magari makubwa, usimamizi wa vyombo vya usafiri, uchukuzi na uhifadhi wa mizigo, usimamizi wa mnyororo wa ugavi, ukaguzi na ukarabati wa magari pamoja na mifumo ya umeme na elektroniki ya magari. Maeneo mengine ni uendeshaji wa maghala na usimamizi wa stoo, uendeshaji wa vituo vya mafuta, ujenzi, usimamizi wa majengo na miundombinu, utalii na ukarimu pamoja na kilimo na uhifadhi wa mazao.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Kasore alisema ushirikiano huo pia utasaidia kuwajengea uwezo wakufunzi na kuhakikisha mafunzo yanayotolewa na VETA yanaendana na mahitaji ya soko la ajira.
Alisema VETA itaendelea kushirikiana na waajiri na wamiliki wa viwanda ili kutambua fursa zilizopo na kuhakikisha wahitimu wanapata nafasi za ajira katika viwanda na maeneo mengine yenye uhitaji wa wataalamu wenye ujuzi.
“Tutahakikisha pia wenzetu wa Van Mo wanapohitaji wataalamu wenye ujuzi mbalimbali, sisi VETA tuweze kusaidia kuwapata. Sambamba na hilo, ushirikiano huu una maslahi mapana kwa wananchi katika kupata fursa za ajira,” alisema Kasore.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Van Mo, Fathi Ahmed Ally, alisema kampuni hiyo imelenga kutoa ajira kwa takribani vijana 500 wenye ujuzi mbalimbali waliohitimu katika vyuo vya VETA.
Alisema kampuni hiyo imeamua kushirikiana na VETA kutokana na ubora wa ujuzi unaopatikana kwa wahitimu wake, hususan katika fani zinazohusiana na shughuli za usafirishaji ambazo ni muhimu katika utekelezaji wa shughuli za kampuni hiyo.
“Kilichotuvutia kuja VETA ni kutokana na wahitimu kutoka katika vyuo hivi kuwa na ujuzi ambao sisi tunauhitaji katika kampuni yetu, hususan shughuli za usafirishaji. Hivyo tumeona hapa ndipo mahali sahihi pa kuwapata vijana wenye ujuzi huo,” alisema Fathi.
EmoticonEmoticon