NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO
WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) umesisitiza matumizi sahihi ya Akili Bandia (AI) na elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) katika kuboresha ubora wa elimu na kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na mahitaji ya karne ya 21.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kuhusu matumizi ya AI na STEM, Mwenyekiti wa Bodi ya ADEM, Dkt. Hillary Dachi, amesema teknolojia hiyo imekuwa sehemu ya maisha ya sasa na ina uwezo wa kubadili namna ya kufundisha, kujifunza na kusimamia elimu.
Amesema AI inaweza kusaidia kuboresha ujifunzaji unaozingatia mahitaji ya mwanafunzi, usimamizi wa taarifa na matumizi ya mbinu bunifu za ufundishaji.
“Akili Bandia si dhana ya siku zijazo tena, bali ni uhalisia unaobadilisha namna tunavyoishi, tunavyofanya kazi na tunavyojifunza,” amesema.
Dkt. Dachi amesema elimu ya STEM nayo ni muhimu katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa kina, kutatua matatizo na kuwa wabunifu, akisisitiza kuwa AI na STEM ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ushindani wa Tanzania katika dunia ya kidijitali.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid Maulid, amesema maendeleo ya teknolojia yameifanya sekta ya elimu kuhitaji viongozi wenye ujuzi wa kidijitali na uwezo wa kutumia teknolojia kwa uwajibikaji.
Amesema AI inaweza kutumika katika utafiti, uchambuzi wa taarifa na takwimu, uandaaji wa vifaa vya kufundishia na kurahisisha baadhi ya shughuli za kiutawala.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, faragha, uadilifu wa kitaaluma na kuepuka utegemezi mkubwa wa teknolojia.
“Tunapaswa kutumia AI kupanua uwezo wa binadamu, na si kuondoa wajibu wa binadamu,” amesema.
Dkt. Maulid amesema mafanikio ya mafunzo hayo yatategemea namna washiriki watakavyotumia maarifa watakayopata katika maeneo yao ya kazi, akiwataka kubaini changamoto na kutumia teknolojia kutafuta suluhisho.
Aidha, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya ushirikiano kati ya ADEM na Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal cha China, uliowekwa rasmi kupitia Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano iliyosainiwa Desemba 29, 2023.
Amesema ushirikiano huo unalenga kuendeleza mafunzo, utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika elimu.
Dkt. Maulid amesisitiza kuwa ADEM itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi katika kujenga uwezo wa viongozi na wataalamu wa elimu.
Kwa upande mwinginee, Dkt. Dachi amewataka washiriki kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya AI na STEM katika taasisi zao na kusambaza maarifa watakayoyapata kwa walimu na jamii.
Amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kujenga mfumo wa elimu unaoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya karne ya 21.
EmoticonEmoticon