TBS YATEKETEZA TANI 3.4 ZA UNGA WENYE SUMUKUVU TABORA NA KIGOMA

August 28, 2026
Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi limeteketeza tani 3.4 za unga wa mahindi wenye sumukuvu (Aflatoxin), wenye thamani ya takribani Sh. milioni 3.5, baada ya vipimo vya maabara kubaini kuwa haukidhi viwango vya usalama kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuteketeza unga huo, Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Hamisi Seleleko Simon, amesema vipimo vya kimaabara vilibaini uwepo wa kiwango kisichokubalika cha sumukuvu, ambacho kinaweza kuhatarisha afya ya walaji.

Amesema matumizi ya chakula chenye sumukuvu kwa kiwango kikubwa yanaweza kusababisha madhara makubwa kiafya, ikiwemo kuongeza hatari ya kupata saratani, hususan saratani ya ini.

“Leo tunafanya zoezi la kuteketeza tani 3.4 za unga wa mahindi wenye sumukuvu kwa kiwango kisichokubalika. Unga huu unateketezwa kwa sababu unaweza kuhatarisha afya ya walaji,” amesema Simon.

Amesema unga huo ni sehemu ya bidhaa zilizozuiwa na TBS wakati wa ukaguzi maalumu uliofanyika katika mikoa ya Tabora na Kigoma mwezi Juni, mwaka 2026.

Kwa mujibu wa Meneja, baada ya bidhaa hizo kuchukuliwa sampuli na kufanyiwa uchunguzi pamoja na vipimo vya kimaabara, ilithibitika kuwa unga huo ulikuwa na sumukuvu na hivyo haukufaa kwa matumizi ya binadamu.

Amebainisha kuwa TBS Kanda ya Magharibi, inayohudumia mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi, itaendelea kutekeleza jukumu lake la kusimamia ubora na usalama wa bidhaa kwa lengo la kulinda afya na usalama wa walaji.

Aidha, ametoa wito kwa wasindikaji, wazalishaji na wafungashaji kuhakikisha bidhaa zao zinathibitishwa ubora na usalama na TBS kabla ya kuziingiza sokoni.

Pia amewataka wamiliki wa maeneo ya kuhifadhia na kuuzia bidhaa za chakula kuhakikisha maeneo yao yanasajiliwa na TBS kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo.

“TBS Kanda ya Magharibi haitasita kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kuwafikisha mahakamani wote watakaobainika kukiuka Sheria ya Viwango na Kanuni zake,” amesema.

Aidha, amewakumbusha walaji kuhakikisha wananunua na kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora na TBS, huku akiwahimiza kutoa taarifa kwa Shirika hilo pindi wanapohisi uwepo wa bidhaa hafifu sokoni.

Amesisitiza kuwa TBS Kanda ya Magharibi itaendelea kufanya ukaguzi katika viwanda, maeneo ya uzalishaji, maghala na masoko mbalimbali ili kuhakikisha bidhaa zinazowafikia wananchi zinakidhi viwango vya ubora na ni salama kwa matumizi.

Kwa upande wake, Meneja wa Ukaguzi na Uzingatiaji wa Sheria wa TBS, Nuru Mwasulama, amesema matumizi ya chakula kilichoandaliwa kwa nafaka iliyochafuliwa na sumukuvu kwa kiwango kikubwa yanaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu.

Mwasulama amesema TBS ina mpango mahususi wa kila mwaka wa kuhakikisha bidhaa zinazopatikana sokoni zinakuwa bora na salama kwa matumizi ya wananchi.

Amesema mpango huo unatekelezwa nchi nzima kupitia ofisi za TBS za kanda, ambapo Shirika hilo lina kanda tisa pamoja na ofisi ndogo kadhaa zinazosaidia kusimamia ubora na usalama wa bidhaa.

“Kupitia kanda hizo, Shirika huendesha mazoezi maalumu ya kupima na kufuatilia ubora wa bidhaa mbalimbali zinazopatikana sokoni ili kubaini bidhaa zisizokidhi viwango na kuchukua hatua stahiki,” amesema Mwasulama.

Amebainisha kuwa ukaguzi huo ni sehemu ya jitihada za TBS kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya bidhaa hafifu zinazoweza kuhatarisha afya na usalama wao.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za TBS katika kulinda afya ya jamii dhidi ya bidhaa zisizokidhi viwango na zinazoweza kusababisha madhara kwa walaji.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »