SAMIA AWEKA SHADA LA MAUA KATIKA KABURI LA ASKARI ASIYEFAHAMIKA URUSI

June 03, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiweka Shada la maua katika Kaburi la Askari Asiyejulikana (Tomb of the Unknown Soldier) pembezoni mwa Ukuta wa Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow nchini Urusi, tarehe 03 Juni, 2026.


…………

Na Beda Msimbe, TBN, Moscow

Kengele kubwa iliyogongwa mara tisa huku bendi ya jeshi ikiongoza nyimbo za maombolezo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan majira ya saa tano na dakika 23 aliweka shada la maua katika kaburi la Askari Asiyefahamika mjini Moscow, Urusi.

Baada ya shughuli hiyo ya uwekaji wa shada la maua katika eneo ambalo moto huwaka daima kama kumbukumbu ya wapiganaji wa Urusi waliopoteza maisha katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, gadi tatu za heshima zilipita kwa mwendo wa haraka kutoa salamu za heshima kwa Rais Samia, sambamba na kupigwa kwa wimbo wa Taifa wa Tanzania.

Nidhamu ya askari waliokuwa katika uwanja huo ilivutia wengi, ambapo walionekana kusimama kwa umakini mkubwa bila kutikisika katika maeneo yao ya ulinzi. Aidha, ubadilishanaji wa gadi pamoja na mwendo wa pole uliomsindikiza Rais Samia kuelekea eneo la uwekaji wa shada la maua viliongeza hadhi na mvuto wa tukio hilo la kihistoria.

Rais Samia ambaye yupo nchini Urusi kwa ziara ya kiserikali, baadaye alikutana na mwenyeji wake, Rais wa Urusi Vladimir Putin, kwa mazungumzo yanayolenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi.

Zaidi ya maofisa 300 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamepata nafasi ya masomo nchini Urusi katika ngazi za shahada ya kwanza na shahada ya pili.

Maofisa hao wamekuwa wakipatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mapambano dhidi ya ugaidi, sayansi na teknolojia, mafunzo ya kijeshi, operesheni za ulinzi wa amani, ununuzi na uhifadhi wa silaha pamoja na namna ya kukabiliana na majanga.

Tanzania na Urusi zinaendelea kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kwa kuzingatia makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi yaliyosainiwa mwaka 2016 pamoja na makubaliano ya ushirikiano wa kifundi wa kijeshi ya mwaka 2018.

Kwa upande mwingine, Tanzania inaendelea kushuhudia ukuaji wa uchumi unaokadiriwa kufikia asilimia 5.5 mwaka 2024 na matarajio ya kufikia asilimia 6 mwaka huu, huku Serikali ikiendelea kusimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kutokana na hali hiyo, ziara ya Rais Samia nchini Urusi inatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi kupitia ajira, biashara, uwekezaji pamoja na ushirikiano wa kiteknolojia na kijeshi kati ya mataifa hayo mawili.

Related StoriesView all

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »