Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameutaka Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuimarisha utoaji wa huduma na kuhakikisha halmashauri inapata uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika Mkutano wa Baraza Maalumu la kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amesisitiza kuwa mapato ndiyo msingi wa uendeshaji wa halmashauri na huwezesha watumishi na madiwani kupata stahiki zao kwa wakati.
Aidha, ameutaka Uongozi wa Halmashauri kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na wananchi wanapata manufaa yaliyokusudiwa kupitia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Kuhusu maagizo ya Kamati za Bunge, RC Mtanda amesema Halmashauri inapaswa kuandaa taarifa za kina kuhusu utekelezaji wa maelekezo hayo badala ya kutoa taarifa za jumla zisizoonyesha hatua zilizofikiwa. Ameongeza kuwa atawaita viongozi husika ili wajieleze kuhusu utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa.
Pia amesisitiza kuwa hoja zote za ukaguzi zilizobaki zinapaswa kujibiwa na kufutwa kwa wakati, akieleza kuwa uwepo wa hoja ambazo hazijafungwa unaathiri taswira ya halmashauri na utendaji wake.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa ametaka madeni yote yanayodaiwa na halmashauri yakusanywe na kulipwa kwa wakati, akibainisha kuwa ukusanyaji wa madeni utachangia kuongeza uwezo wa kifedha na kuwezesha utekelezaji wa miradi zaidi ya maendeleo.
Vilevile, amewahimiza Viongozi kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi mbalimbali vya kiuchumi ili waweze kukidhi vigezo vya kupata mikopo kutoka halmashauri na taasisi za fedha, hatua itakayosaidia kuongeza shughuli za uzalishaji na kuinua uchumi wa wananchi.
Akihitimisha RC Mtanda pia amewapongeza Wahe. Madiwani wa halmashauri hiyo na kuwataka kuendelea kuhamasisha wananchi kudumisha amani na utulivu, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya amani na mshikamano katika jamii.




EmoticonEmoticon