RAIS VLADMIR PUTIN: URUSI KUFUNGUA FURSA MPYA ZA UCHUMI TANZANIA

June 03, 2026

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin pamoja na ujumbe wake katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Ikulu ya Kremlin jijini Moscow nchini Urusi tarehe 03 Juni, 2026.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.

…………. 

Na Beda Msimbe, TBN, Moscow

Urusi imesema itaendelea kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa Tanzania kwa manufaa ya pande zote mbili katika kuimarisha ushirikiano wa maendeleo.
Aidha, taifa hilo lenye jumla ya miradi 70 nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 434.22, ambayo imewezesha ajira zaidi ya 3,018, limesema litazitangaza zaidi fursa hizo katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaotarajiwa kufanyika kesho kutwa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao chake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema taifa lake limekuwa likifuatilia kwa karibu mageuzi mbalimbali yanayofanyika nchini Tanzania na kuridhishwa na kasi ya maendeleo yake.
Putin amesema mazungumzo yake na Rais Samia yamekuwa yenye manufaa makubwa kwa mataifa yote mawili na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Urusi na Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake, Rais Samia amesema ziara yake katika Shirikisho la Urusi ina umuhimu mkubwa wa kihistoria kwake binafsi na kwa taifa la Tanzania kwa ujumla.
“Ziara yangu ina umuhimu wa pekee wa kihistoria kwangu binafsi na kwa nchi yangu. Imepita zaidi ya nusu karne tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiserikali ya Tanzania nchini Urusi. Hivyo, kwangu hii ni safari ya kihistoria sana kuja Urusi kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili pamoja na maendeleo endelevu kwa wananchi wetu. Kwa niaba yangu na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa mwaliko huu,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alikumbusha mchango mkubwa wa Urusi katika harakati za Tanzania za kupigania uhuru na kumpongeza Rais Putin kwa maadhimisho ya miaka 81 ya ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia yaliyofanyika Mei 9 mwaka huu.
Rais Samia aliwasili jijini Moscow kwa ziara yake ya kwanza nchini Urusi, ambayo pia ni ziara ya kwanza ya kiongozi wa Tanzania nchini humo katika kipindi cha zaidi ya miaka 50, kwa ajili ya mazungumzo rasmi na Rais Putin.
Kwa mujibu wa viongozi hao, mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi. Vilevile, walibadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa mataifa yao.      

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »