ORYX GAS YAADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI KWA KUFANYA USAFI SOKO LA FERI

June 05, 2026

Kampuni ya Oryx Gas imeadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kufanya usafi katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri jijini Dar es Salaam na kukabidhi vifaa vya usafi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi.

Akizungumza leo Juni 5,2026 wakati wa shughuli hiyo, Meneja wa Masoko na Mauzo wa Oryx Gas, Shaban Fundi, amesema kampuni hiyo imeamua kutumia maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kutumia nishati safi.

Amesema Oryx inaamini kuwa mazingira safi yanachangia afya bora, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu, ndiyo maana imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza kampeni za usafi na uhifadhi wa mazingira.

“Leo tumeungana na wafanyabiashara wa Soko la Feri kufanya usafi wa mazingira na kukabidhi vifaa vitakavyosaidia kuendeleza usafi huu hata baada ya maadhimisho. Lengo letu ni kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa safi na salama kwa kila anayefanya shughuli zake hapa,” alisema Fundi.

Ameongeza kampuni hiyo pia inaendelea kuhamasisha matumizi ya gesi kama nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa matumizi ya gesi yanasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao ni miongoni mwa sababu zinazochangia uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake, Meneja wa Soko la Kimataifa la Samaki Feri Suleiman Mfinanga ameishukuru Oryx Gas kwa mchango wake katika kuboresha mazingira ya soko hilo, akisema hatua ya kufanya usafi na kutoa vifaa vya usafi imeonyesha mfano mzuri wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na jamii.

Amesema soko hilo linapokea idadi kubwa ya wafanyabiashara na wateja kila siku, hivyo usafi ni jambo muhimu katika kuhakikisha shughuli za biashara zinafanyika katika mazingira salama na yenye afya.

“Tunawashukuru Oryx kwa kutuchagua katika maadhimisho haya. Vifaa walivyotukabidhi vitatusaidia kuendelea kudumisha usafi wa soko letu na kuwajengea wafanyabiashara utamaduni wa kutunza mazingira,” alisema.

Naye mfanyabiashara wa soko hilo, Mwanahawa Noel, alisema shughuli hiyo imeongeza hamasa kwa wafanyabiashara kuendelea kushiriki katika usafi wa mazingira na kuhakikisha soko linabaki katika hali nzuri wakati wote.

Kwa upande wake, Shaibu Ulaya alisema uwepo wa Oryx katika soko hilo umeleta manufaa makubwa, si tu kupitia matumizi ya gesi bali pia katika kuhamasisha usafi na utunzaji wa mazingira.

Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira na kutumia nishati safi ili kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »