MRADI WA FUNZA WACHANGIA UHIFADHI WA MAZINGIRA NA UFUGAJI

June 04, 2026

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeendelea kuwaibua na kuwawezesha wabunifu nchini kupitia mafunzo yanayolenga kugeuza ubunifu wao kuwa fursa za ajira na maendeleo ya kiuchumi.

Miongoni mwa wabunifu hao ni Dkt. Lucas Luchemba kutoka Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), ambaye ameanzisha mradi wa ufugaji wa wadudu aina ya inzi chuma au kwa jina lingine (Black Soldier Fly) unaolenga kutatua changamoto ya uhaba wa protini katika chakula cha mifugo sambamba na kuchangia utunzaji wa mazingira kupitia matumizi ya taka ozo.

Mradi huo hutumia mabaki ya chakula, maganda ya matunda na taka nyingine zinazooza kama chakula cha wadudu hao, ambao huzalisha funza wenye kiwango kikubwa cha protini kinachofikia asilimia 40 hadi 50. Funza hao hutumika kutengeneza chakula cha samaki, kuku na mifugo mingine.

Akizungumza kuhusu ubunifu huo, Dkt. Luchemba amesema alibaini changamoto ya utegemezi mkubwa wa samaki na soya kama vyanzo vikuu vya protini katika chakula cha mifugo, huku bidhaa hizo zikitumika pia kwa matumizi ya binadamu, hali inayoongeza gharama na ushindani wa upatikanaji wake.

“Tumekuja na mbadala wa protini unaotumia rasilimali zinazopatikana kwa urahisi kupitia taka zinazooza, ambazo kwa kawaida hutupwa na kusababisha uchafuzi wa mazingira,” amesema.

Ameeleza kuwa taka kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo vyuoni, masokoni, kwa mama lishe na wauza chipsi hukusanywa na kuchakatwa kabla ya kutumika kulisha wadudu hao. Hatua hiyo husaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira, harufu katika madampo na uzalishaji wa gesi hatari zinazotokana na taka zinazooza. 

Kwa mujibu wa Dkt. Luchemba, mradi huo una manufaa makubwa mawili; kuzalisha protini mbadala kwa ajili ya chakula cha mifugo na kupunguza kiasi cha taka zinazoharibu mazingira.

Mbali na kuzalisha funza, tayari mradi huo umeanza mchakato wa kutengeneza chakula cha samaki na kuku kwa kutumia protini inayotokana na wadudu hao badala ya unga wa samaki au soya zinazotumika kwa kiwango kikubwa kwa sasa. 

Ameeleza kuwa ubunifu huo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha tafiti zinazofanyika vyuoni zinatoa suluhisho la moja kwa moja kwa changamoto zinazoikabili jamii.

Kutokana na mafanikio ya mradi huo, Dkt. Luchemba amesema amepata hati miliki kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), hatua ambayo imeimarisha ulinzi wa teknolojia na ubunifu huo.
Hata hivyo, amesema bado wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali ili kupanua mradi huo kwa kupata eneo kubwa zaidi karibu na dampo, mashine za kuchakata taka, vifaa vya kukaushia funza pamoja na usafiri wa kukusanya taka kutoka maeneo tofauti.

Amesema lengo lao ni kufikia uwezo wa kuzalisha tani 10 za funza kwa mwezi ili kukidhi mahitaji ya wafugaji wa samaki, kuku na mifugo mingine nchini.

Aidha, mradi huo unatumika kama shamba darasa kwa wanafunzi, wanawake na vijana wanaotaka kujifunza namna ya kutumia taka kuzalisha fursa za kiuchumi huku wakichangia uhifadhi wa mazingira.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »