MRADI MPYA WA UMEME KONGWA KULETA AHUENI KWA WAMILIKI WA VIWANDA

June 16, 2026




Na Mwandishi Wetu


Wamiliki wa viwanda vidogo katika Wilaya ya Kongwa wameeleza matumaini makubwa ya kuondokana na changamoto ya umeme mdogo (low voltage) na mgao wa umeme kufuatia kuzinduliwa kwa mradi mpya wa miundombinu ya umeme utakaoimarisha upatikanaji wa nishati katika eneo hilo.


Mradi huo unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya kilovoti 33 (33kV) kutoka Zuzu hadi Mbande yenye urefu wa kilomita 32 pamoja na kituo cha kubadilisha na kusambaza 

umeme chenye uwezo wa MVA 20, kitakachoboresha huduma za umeme katika wilaya za Kongwa, Chamwino na maeneo jirani.

Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa viwanda hivyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika leo Juni 16, 2026, Mbande wilayani Kongwa, Mjumbe wa Umoja wa Viwanda Vidogo Wilaya ya Kongwa na mwakilishi wa mwenyekiti wa umoja huo, Nemes Adam Mtei, amesema tatizo la umeme lilikuwa likisababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara.

"Tumekuwa na shida kubwa sana ya umeme mdogo usioridhisha, hali iliyosababisha kuungua kwa mota za mashine zetu na kupunguza uzalishaji. Tunamshukuru sana Waziri kwa kutuletea mradi huu ambao tunaamini utabadilisha maisha ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla," amesema Mtei.


Mtei, ambaye pia ni mkazi wa Kibaigwa, amepongeza Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa kuzindua mradi huo na kumshukuru  Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, kwa usimamizi uliowezesha kukamilika kwa mradi huo wenye thamani ya Sh.bilioni 10.5.


Amesema mradi huo uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu sasa utafungua fursa mpya za uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa viwanda vidogo na kukuza uchumi wa wananchi wa Kongwa na maeneo ya jirani.


&&&

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »