Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW) kimetangaza kufanyika kwa Kongamano lake la Kwanza la Kimataifa la Uwezeshaji wa Watu na Ustawi wa Jamii, litakalofanyika Juni 5, 2026 katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Joyce Nyoni, alisema kongamano hilo lenye kauli mbiu ya “Kuwawezesha Watu na Kubadilisha Jamii: Njia za Kufikia Ustawi Endelevu” litawakutanisha wataalamu, watafiti, watunga sera na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Dkt. Nyoni alisema washiriki kutoka nchi 11, zikiwemo Tanzania, Uganda, Kenya, Nigeria, Namibia, Afrika Kusini, Norway na Hungary, wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo ambalo litafunguliwa rasmi na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima.
Alisema kongamano hilo litatumika kama jukwaa la kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu mbalimbali za kushughulikia changamoto za kijamii na kiuchumi zinazokabili jamii, huku likilenga kuimarisha ustawi wa wananchi na maendeleo jumuishi.
Kwa mujibu wa chuo hicho, mada mbalimbali zitawasilishwa na wataalamu mashuhuri kutoka nchi sita, zikijikita katika masuala ya ustawi wa jamii, usawa wa kijinsia, maendeleo ya watoto, afya ya akili, ujasiriamali na uwezeshaji wa wananchi.
Dkt. Nyoni alisema kongamano hilo linafanyika katika kipindi muhimu wakati Tanzania ikielekea kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga jamii yenye ustawi, fursa sawa na maendeleo jumuishi kwa wananchi wote.
Aliongeza kuwa mapendekezo yatakayozalishwa kupitia tafiti, mijadala na mawasilisho ya kongamano hilo yatawasilishwa kwa wizara na taasisi husika ili yaweze kutumika kama mchango wa kitaalamu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, aliwataka wananchi, wanataaluma na wadau mbalimbali wa maendeleo kufuatilia kongamano hilo kupitia mifumo ya mtandao, akisema matokeo yake yanatarajiwa kuchangia kuboresha sera, mipango na mikakati ya maendeleo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.





EmoticonEmoticon