FIDIA ZAANZA KUMWAGIKA PANGANI, WANANCHI 474 KUPISHA MRADI WA SUKARI WA DOLA MILIONI 350

June 26, 2026

 




Na Oscar Assenga, Pangani

SERIKALI imeanza rasmi kulipa fidia kwa wananchi 474 wa vijiji vya Mseko na Kigurusimba, Kata ya Masaika, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, kupisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari wenye thamani ya dola za Marekani milioni 350.

Hatua hiyo inaashiria mwanzo wa utekelezaji wa moja ya miradi mikubwa ya uwekezaji nchini inayotarajiwa kuzalisha maelfu ya ajira, kuongeza uzalishaji wa sukari na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Wilaya ya Pangani na taifa kwa ujumla.

Akizindua rasmi zoezi la ulipaji fidia, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Burian, alisema Serikali imeanza kuwalipa wananchi wote waliokamilisha taratibu zinazohitajika ili kuondoa vikwazo vya utekelezaji wa mradi huo.

Alisema zaidi ya wananchi 400 tayari wamekamilisha kusaini nyaraka zinazowaruhusu kupokea malipo yao, huku akibainisha kuwa waliojitokeza mapema watapewa kipaumbele na wengine wataendelea kuhudumiwa kadri watakavyokamilisha taratibu.

"Tunataka zoezi hili lifanyike kwa uwazi, haki na kwa wakati. Serikali imejipanga kuhakikisha kila mwananchi aliyestahili analipwa fidia yake bila kuchelewa," alisema Dkt. Burian.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka zinazoratibu zoezi hilo ili kuhakikisha mradi unaanza kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa jamii na taifa.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Remigius Reverius alisema malipo yanafanyika moja kwa moja kupitia akaunti za benki za wanufaika waliokamilisha uhakiki wa nyaraka zao.

Alisema zoezi hilo limeanza katika Kijiji cha Kigurusimba na litaendelea kwa awamu hadi wananchi wote waliothibitishwa kulipwa fidia watakapopokea stahiki zao.

"Tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao. Serikali kupitia TISEZA imejipanga kuhakikisha kila aliyefanyiwa tathmini analipwa haki yake. Zoezi hili litaendelea hadi Juni 30 mwaka huu," alisema Reverius.

Aliongeza kuwa wataalamu wanaendelea kuhakiki taarifa za akaunti za benki pamoja na nyaraka mbalimbali ili kuhakikisha malipo yote yanafanyika kwa usahihi na bila dosari.

Mwakilishi wa wakulima wa Kigurusimba, Biligita Batilimeo, alisema kuanza kwa ulipaji wa fidia ni hatua muhimu inayoonyesha dhamira ya Serikali ya kutekeleza mradi huo huku ikilinda maslahi ya wananchi.

Alisema pamoja na fidia, mradi huo unatarajiwa kufungua fursa nyingi za ajira na biashara ambazo zitainua uchumi wa wakazi wa Pangani.

Naye mkazi wa Kigurusimba, Benard Mhagama, aliwasihi wananchi watakaopokea fidia kutumia fedha hizo kwa busara kwa kuwekeza katika shughuli za maendeleo zitakazowanufaisha wao na familia zao kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Masaika, George Mariano, alisema uwekezaji huo utabadilisha sura ya uchumi wa Pangani kwa kuongeza ajira, kuchochea shughuli za biashara na kuongeza mapato ya Serikali.

Mradi huo wa kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari unatekelezwa na TISEZA katika eneo la ekari 22,000 kwa gharama ya dola za Marekani milioni 350, na unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa itakayochangia kuongeza uzalishaji wa sukari nchini pamoja na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Tanga.

Mwisho.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »