DCEA, VETA Kuibua Matumaini Mapya kwa Waraibu Waliopona

June 04, 2026

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) zimeingia makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha waraibu waliopona matumizi ya dawa za kulevya kupata mafunzo ya ufundi stadi, hatua inayolenga kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kuzuia kurejea kwenye matumizi ya dawa hizo.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo leo Juni 4, 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini, ikiwemo kuzuia biashara haramu ya dawa hizo, kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuimarisha huduma za tiba na urejeshaji wa waraibu.

Alisema ushirikiano huo umetokana na kutambua umuhimu wa kuwawezesha waraibu waliopona kupata ujuzi wa kujiajiri na kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

“Ushirikiano na VETA ni mfano mzuri wa namna taasisi za serikali zinavyoweza kushirikiana katika kutatua changamoto za kijamii kwa manufaa ya taifa,” alisema Lyimo.

Alieleza kuwa waraibu wengi wanaopata nafuu hujikuta wakirejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kukosa shughuli za kufanya au njia mbadala za kujipatia kipato. Kwa sababu hiyo, mafunzo ya ufundi stadi yatawasaidia kujenga maisha mapya na kuondokana na mazingira yanayoweza kuwarudisha kwenye uraibu.

Lyimo alisema baada ya kuhitimu mafunzo hayo, wahitimu watawezeshwa kwa vifaa vya msingi vya kuanzia kazi kulingana na taaluma walizosomea, pamoja na kuunganishwa na taasisi za fedha zinazotoa mikopo midogo midogo ili kupata mitaji ya kuanzisha biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Aidha, alisema ushirikiano huo unaendana na mradi wa Serikali wa ujenzi wa kituo kikubwa cha urejeshaji na mafunzo kwa waraibu katika Jiji la Dodoma. Kituo hicho kitatoa mafunzo ya ufundi stadi kwa mfumo wa VETA kwa waraibu waliopata nafuu na kuthibitishwa kuwa wana uwezo wa kuendelea na masomo.

Kwa mujibu wa DCEA, waraibu wanaopata matibabu katika kliniki, nyumba za uangalizi maalumu (Sober Houses), hospitali za rufaa na za kanda watapimwa maendeleo yao, na watakapothibitishwa kuwa wamepona kwa kiwango kinachowaruhusu kujifunza, wataelekezwa katika kituo hicho cha Dodoma au kwenye vituo vingine vya VETA nchini.

Ili kuimarisha mchakato huo, DCEA imeanzisha kitengo maalumu cha Social Welfare Recovery Response chenye jukumu la kufuatilia ustawi wa waraibu waliopona, kuwaunganisha na jamii, kuwasaidia kupata mikopo na fursa za ujasiriamali pamoja na kusimamia matumizi ya mitaji wanayopata.

DCEA imeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha mamlaka hiyo na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali za serikali, hatua itakayosaidia waraibu waliopona kurejea katika maisha ya kawaida na kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore, alisema ushirikiano huo unalenga kuwapa fursa waraibu waliopata nafuu na kuthibitishwa kuwa tayari kwa mafunzo ili wapate ujuzi utakaowawezesha kujitegemea kiuchumi.

Alisema wahitimu watakuwa na uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa au kuanzisha vikundi vya uzalishaji vitakavyotoa ajira kwa wengine, huku wakitambuliwa rasmi kwa vyeti vitakavyotolewa baada ya kuhitimu mafunzo hayo.

Kasore alibainisha kuwa vyeti hivyo vitawawezesha wahitimu kupata fursa mbalimbali za mikopo kutoka serikalini na taasisi za kifedha, hatua itakayowasaidia kuanzisha miradi na biashara za kuongeza kipato.

Aliongeza kuwa uwekezaji katika elimu ya ufundi stadi ni sehemu muhimu ya kuwawezesha vijana kujenga maisha bora na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

VETA pia imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma katika kukabiliana na changamoto za kijamii, huku ikiwataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwahamasisha vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ili kujenga mustakabali wenye tija.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »