SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limesema linaendelea kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kitaifa yanayofanyika mkoani Iringa kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya maziwa na wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango na ubora wa bidhaa za maziwa.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Udhibiti ubora kutoka shirika la viwango (TBS) Timotheo Mwendi amesema kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kusimamia viwango na ubora wa bidhaa mbalimbali nchini ikiwemo maziwa na bidhaa zake, vyakula pamoja na vinywaji vingine.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kutumia bidhaa za maziwa zenye alama ya ubora ya TBS kwani ni uthibitisho kuwa bidhaa hizo zimekaguliwa na kukidhi viwango vinavyotakiwa.
Meneja mauzo wa Kampuni ya Shafa Farms Kalila Salando amesema kampuni hiyo inazingatia viwango vyote vya uzalishaji wa maziwa kwa kufuata maelekezo na miongozo inayotolewa na taasisi mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa ubora na usalama wa vyakula nchini, ikiwemo TBS.
Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kitaifa yanayoendelea mkoani Iringa yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi tarehe 1 Juni 2026, baada ya wiki nzima ya shughuli mbalimbali zilizolenga kuhamasisha uzalishaji, usindikaji na matumizi ya maziwa bora na salama nchini.





EmoticonEmoticon