QWARAY AVUTIWA NA UBUNIFU WA TEHAMA RIDC

May 20, 2026


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Ndege Qwaray (Mb), amefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (Research, Innovation and Development Centre – RIDC) kilichopo jijini Dodoma, ambapo amekagua miradi mbalimbali ya TEHAMA inayotekelezwa na kituo hicho kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma Serikalini.

Katika ziara hiyo iliyofanyika mapema wiki hii, Mhe. Qwaray alipata fursa ya kutembelea na kujionea miradi ya kiteknolojia inayolenga kutoa suluhisho kwa changamoto katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na utawala.

Aidha, miradi hiyo inahusisha matumizi ya teknolojia zinazochipukia kama vile Internet of Things (IoT) na Akili Mnemba (AI), katika kurahisisha utendaji kazi Serikalini na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Qwaray ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa juhudi zake za kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana, kupitia tafiti na ubunifu wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

“Niwapongeze e-GA kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kukuza ubunifu na tafiti za teknolojia. Dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kubwa kutokana na maendeleo ya teknolojia, hivyo ni muhimu kuendelea kujifunza, kufanya tafiti na kubuni mifumo mipya itakayokwenda sambamba na mabadiliko hayo,” amesema Mhe. Qwaray.

Amesisitiza kuwa, bunifu zote zinazotengenezwa zinapaswa kuwa na tija kwa jamii na kuchangia moja kwa moja katika kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi pamoja na kuongeza ufanisi ndani ya taasisi za Serikali.

Sambamba na hilo, Mhe. Qwaray amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya e-GA, vyuo vikuu na sekta binafsi ili kuongeza uwekezaji katika tafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia zinazoweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa e-GA, Mhandisi Benedict Ndomba, amesema kituo hicho kimeendelea kuwa chachu ya mageuzi ya kidijitali Serikalini kupitia ujenzi wa mifumo mbalimbali inayotumika katika taasisi za umma.

Ametaja baadhi ya mifumo hiyo kuwa ni Mfumo wa Uendeshaji wa Vikao vya Bodi na Menejimenti (e-Board) pamoja na Mfumo wa Uendeshaji wa Vikao Kidijitali (e-Mikutano), ambayo imekuwa ikisaidia kuongeza ufanisi katika shughuli za Serikali.

“Kituo hiki kimekuwa na manufaa makubwa kwa taifa kutokana na kazi zake za utafiti, ubunifu na maendeleo ya mifumo ya TEHAMA. Pia, kimefungua fursa kwa wanafunzi na vijana wenye taaluma ya TEHAMA kushiriki katika tafiti na bunifu mbalimbali kwa maslahi ya taifa,” amesema Mha.Ndomba.

Katika kuonesha dhamira ya Serikali kuendelea kuimarisha kituo hicho, Mhe. Qwaray ameahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na e-GA kutatua changamoto zinazoikabili RIDC ili kuongeza fursa kwa vijana wengi zaidi wa Kitanzania kupata nafasi ya kujifunza, kufanya tafiti na kushiriki katika ubunifu wa teknolojia mbalimbali za kisasa.







Share this

Related Posts

Previous
Next Post »