NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imezindua maabara za kompyuta katika Shule ya Sekondari Kimara pamoja na Shule ya Msingi Mkwawa jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo na jitihada za kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta ya elimu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Mei 16, 2026 jijini Dar es Salaam, Afisa Tawala wa Manispaa ya Ubungo, Diana Kalimuna aliyemwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema vifaa hivyo vitawasaidia wanafunzi kujenga uwezo wa kutumia teknolojia ya kisasa na kukabiliana na ushindani wa dunia ya kidijitali.
Amesema matumizi sahihi ya TEHAMA katika elimu yataongeza ubunifu, ufanisi wa ujifunzaji pamoja na kuwaandaa wanafunzi kuwa na maarifa yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa.
Aidha, amewataka walimu na wanafunzi kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa vizuri ili viweze kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Kalimuna amepongeza uongozi wa TET kwa ushirikiano mkubwa na mchango wake katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo wa maabara za kisasa za kujifunzia.
Pamoja na hayo, amesema amepokea maombi mbalimbali kutoka kwa walimu na uongozi wa shule kuhusu changamoto ya upungufu wa walimu pamoja na mazingira ya makazi yao, na kuahidi kuyafanyia kazi pamoja na kutoa mrejesho kwa uongozi wa shule hizo.
“Pia kuhusu mafunzo ya walimu kwenda nchini Korea, nimefarijika kuona viongozi wetu wa Wilaya ya Ubungo wameonesha nia ya kulifuatilia jambo hilo. Nami nitashirikiana nao kuhakikisha linapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili walimu wetu wapate nafasi ya kuongeza ujuzi na uzoefu,” amesema Kalimuna.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dkt. Aneth Komba amesema kila shule imepokea vifaa mbalimbali vya TEHAMA ikiwemo seti 26 za kompyuta, mashine ya kutoa nakala, skrini ya projekta, projekta ya HD pamoja na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia.
Vifaa vingine vilivyotolewa ni pamoja na StandbyMe “Elektroniki Podium”, MotionDesk, mausi na kibodi zisizo na waya kwa mwalimu, “Electronic Pointer” pamoja na amplifaya.
Dkt. Komba amesema maabara hizo ni matokeo ya programu ya Korean e-Learning Improvement Cooperation (KLIC) yenye lengo la kuwajengea uwezo walimu kufundisha kwa kutumia TEHAMA na kuhakikisha shule zinakuwa na vifaa vya kisasa vya kielektroniki kwa ajili ya ujifunzaji na ufundishaji.
“Hii ni programu yenye lengo la kuwajengea uwezo walimu kufundisha kwa kutumia TEHAMA na kuhakikisha shule zetu zinakuwa na vifaa vya kisasa vya kielektroniki kwa ajili ya ujifunzaji na ufundishaji,” amesema.
Aidha, amesema kupitia programu hiyo walimu wamekuwa wakipata fursa ya kushiriki mafunzo nchini Korea Kusini ili kuongeza ujuzi na uzoefu katika matumizi ya TEHAMA darasani.
Kwa mwaka huu, walimu kutoka Shule ya Sekondari Kimara na Shule ya Msingi Mkwawa wanatarajiwa kushiriki mafunzo hayo, hatua ambayo itasaidia kuimarisha matumizi ya TEHAMA na Akili Unde katika ufundishaji na ujifunzaji.
Amesisitiza kuwa TET itaendelea kutoa mafunzo na usimamizi wa karibu ili kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika ipasavyo na kuwanufaisha walimu pamoja na wanafunzi.












EmoticonEmoticon