Serikali kupitia Wizara ya Nishati imetenga shilingi milioni 273.6 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusambaza umeme wa jua katika visiwa saba vya Wilaya ya Musoma ikiwemo Nyasaungu, Muroba, Kagongo, Nyamasanje, Rukuba na Iriga, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Rais, Mhe. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya umeme bila kujali eneo analoishi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ya kutatua kero za wananchi katika Jimbo la Musoma Vijijini.
Amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika upatikanaji wa umeme ambapo vijiji vyote katika jimbo hilo tayari vimefikiwa na huduma hiyo, huku hatua zinazofuata zikielekezwa katika kufikisha umeme kwenye vitongoji vilivyosalia.
Amebainisha kuwa kati ya vitongoji 374 vilivyopo, takribani 100 pekee ndivyo bado havijafikiwa na umeme huku zaidi ya vitongoji 50 vikiwa katika hatua za utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme.
Aidha, amesema Serikali imepokea maombi ya Mbunge wa Musoma Vijijini ya kuhakikisha vitongoji vyote ambavyo havina umeme vinafikiwa na huduma hiyo ifikapo mwaka 2027, akieleza kuwa lengo hilo linaendana na dhamira ya Serikali inayolenga kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinaunganishwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.
Sambamba na hilo, Mhe. Salome amesema Wizara ya Nishati imeendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya uzalishaji mali, ikiwemo maeneo ya wachimbaji wa migodi wilayani Musoma Vijijini.
Kuhusu baadhi ya wananchi ambao miundombinu ya umeme imepita karibu na makazi yao lakini hawajaunganishwa na huduma hiyo, amemuelekeza Meneja wa TANESCO Wilaya ya Musoma kuhakikisha wananchi hao wanaunganishiwa umeme.
Katika hatua nyingine, amewahimiza wananchi wa Musoma Vijijini kutumia nishati safi ya kupikia, akibainisha kuwa Serikali imetoa ruzuku ya zaidi ya asilimia 50 kwenye majiko ya gesi ili kuyawezesha kupatikana kwa gharama nafuu.










EmoticonEmoticon