WITO umetolewa kwa viongozi wa Serikali za Mitaa nchini kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Elimu Tanzania(TEA) katika uanzishwaji na uendeshaji wa Mifuko ya Elimu ya Halmashauri ili kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta ya elimu.
Wito huo umetolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia wasilisho lililofanyika katika Mkutano Mkuu Maalum wa Viongozi wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), uliofanyika Aprili 22, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. George Mofulu, Meneja wa Utafutaji Rasilimali na Hamasa aliwasilisha mada iliyoeleza nafasi ya TEA katika kuendeleza sekta ya elimu nchini kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.
Kuhusu mafanikio ya Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na TEA, amesema jumla ya miradi 1,711 yenye thamani ya shilingi bilioni 128.5 imetekelezwa katika kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka wa fedha 2014/15 hadi 2024/25.
Katika mkutano huo, TEA pia ilikumbusha kuhusu Waraka wa Serikali Na. 1046 na 1047 wa mwaka 2020 unaozitaka Halmashauri kuanzisha, kuendesha na kusimamia Mifuko ya Elimu ya Halmashauri. Tathmini ya mwaka 2025 ilibaini kuwa zaidi ya asilimia 76 ya Halmashauri bado hazijatekeleza kikamilifu jukumu hilo.
Kutokana na hali hiyo, TEA imesisitiza umuhimu wa Halmashauri kuchukua hatua madhubuti za kuanzisha mifuko hiyo ili kuongeza vyanzo vya ndani vya rasilimali kwa ajili ya kuendeleza elimu kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali waliopo katika maeneo yao.
Akihitimisha wasilisho hilo, Dkt. Mofulu alieleza kuwa TEA ipo tayari kushirikiana na Halmashauri zote nchini katika kuanzisha na kuendesha Mifuko ya Elimu kwa ufanisi.
#TEA #ALAT2026 #ElimuTanzania #MfukoWaElimu #TawalaZaMitaa Arusha AICC MaendeleoYaElimu

EmoticonEmoticon