NYASI BANDIA SULUHISHO LA KUDUMU UWANJA WA CCM MKWAKWANI

April 11, 2026



Na Oscar Assenga, Tanga

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimeeleza kuwa suluhisho la kudumu la kuboresha eneo la kuchezea katika Uwanja wa CCM Mkwakwani ni uwekaji wa nyasi bandia, huku wakipanga kushirikiana na wadau wa soka kufanikisha mpango huo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua uwanja huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdurahman, alisema uwekaji wa nyasi bandia unakadiriwa kugharimu kati ya shilingi milioni 400 hadi 500.

Ziara hiyo ni sehemu ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo, ikiwemo ile inayotekelezwa kwa fedha zinazotolewa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kupunguza kero kwa wananchi.

Abdurahman aliwataka viongozi wa CCM, ambao ni wamiliki wa uwanja huo, kutumia ubunifu na kushirikiana na wadau wa soka ili kuhakikisha wanapata fedha za kuweka nyasi bandia.

“Tutawaomba wadau wa soka nchini watakapohitajika kutusaidia, kwani dhamira yetu ni njema. Kama ambavyo wamekuwa wakitusaidia hapo awali, tunaamini watashiriki nasi kuhakikisha tunakuwa na uwanja wa kisasa zaidi,” alisema.

Alieleza kuwa maboresho ya uwanja huo yatasaidia kuinua uchumi wa Mkoa wa Tanga, kwani utaweza kutumika kwa mashindano ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo CECAFA na michuano mingine ya Afrika.

“Tunapokuwa na uwanja mzuri, hata timu za nje zitakuja kucheza hapa Tanga. Hii itaongeza mzunguko wa fedha na kukuza uchumi wa mkoa wetu,” aliongeza.

Aidha, alikumbusha kuwa uwanja huo uliwahi kufungiwa kutokana na kutokidhi vigezo, hasa ubora wa eneo la kuchezea, akisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa sasa zinalenga kuhakikisha viwango vinazingatiwa kwa usalama wa wachezaji na ubora wa mchezo.

“Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapofungia uwanja si kwa kupenda, bali kuhakikisha viwango vinazingatiwa. Ndiyo maana tumekuwa wepesi kuchukua hatua za maboresho,” alisema.

Katika hatua nyingine, Abdurahman alieleza kuridhishwa na maendeleo ya ufungaji wa viti 6,500 vilivyotolewa na TFF chini ya Rais wake, Wallace Karia, licha ya kuwepo kwa ucheleweshaji mwanzoni.

Amesema tayari ameagiza kazi hiyo ikamilike ndani ya mwezi mmoja, na kwa sasa inaendelea vizuri chini ya usimamizi wa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa, Nasoro Makau.

Kwa mujibu wa mpango huo, maeneo ya kipaumbele ni jukwaa kuu pamoja na sehemu za mashabiki wa klabu za Coastal Union na African Sports. Pia wameomba viti vingine 2,500 ili kukamilisha uwanja mzima.

Abdurahman aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, inayoongozwa na Waziri Paul Makonda na Naibu wake Hamisi Mwinjuma, pamoja na Rais wa TFF Wallace Karia, kwa ushirikiano wao katika kuboresha uwanja huo.

Alisisitiza kuwa maboresho hayo yanalenga kuhakikisha klabu za Coastal Union na African Sports zinaendelea kucheza mechi zao za nyumbani mkoani Tanga badala ya kuhamishiwa maeneo mengine.

Aidha, aliwataka mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi uwanjani kuunga mkono timu zao.

“Haileti maana kuwa na uwanja mzuri halafu mashabiki wanabaki nyumbani kuangalia mechi,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa Uwanja wa Mkwakwani, Nasoro Makau, alisema hadi sasa wamefikia asilimia 40 ya ufungaji wa viti na wana uhakika wa kukamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »