MWANAMKE CHUMA MAENDELEO GROUP YAWAKUMBUKA WAFUNGWA WANAWAKE GEREZA LA KAHAMA

April 10, 2026

Na Kadama Malunde - Kahama

Katika kuendeleza jitihada za kijamii na kuonesha mshikamano wa dhati kwa wanawake wenzao, Kikundi cha wanawake maarufu kinachojulikana kama Mwanamke Chuma Maendeleo Group kimetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wafungwa wanawake katika Gereza la Kahama Mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea kilele cha Tamasha la Mwanamke Chuma 2026 litakalofanyika Aprili 11, 2026 Mjini Kahama.

Msaada huo uliokabidhiwa unajumuisha mahitaji muhimu ya kila siku kama vile sabuni, taulo za kike, dawa za meno, nguo, lishe ya watoto, kandambili (ndala) pamoja na mafuta ya kujipaka ikiwa ni hatua ya kupunguza changamoto ndogondogo zinazowakabili wafungwa hao na wakati huo huo kuwapa faraja ya kihisia.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo Ijumaa Aprili 10,2026 , Mwenyekiti wa Mwanamke Chuma Maendeleo Group, Bi. Neema Moshi, amesema kuwa hatua hiyo inatokana na dhamira ya kundi hilo kuhakikisha kuwa wanawake wote, bila kujali walipo, wanapata faraja na kuendelea kuamini katika thamani yao.
Neema Moshi akizungumza

“Tukiwa na kaulimbiu ya ‘Nguvu ya Ujasiri’, tumeona ni muhimu kuwafikia wanawake wenzetu waliopo gerezani ili kuwatia moyo na kuwaonesha kuwa hawako peke yao. Tumekuja kama wawakilishi wa wanachama wetu kuwapa ujumbe wa matumaini na mshikamano,” amesema Bi. Moshi.

Kwa upande wake, Mwandaaji wa Tamasha la Mwanamke Chuma 2026 ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Redio cha Gold FM, Bi. Neema Mghen, amesisitiza kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kuhamasisha matumaini na ujasiri kwa wanawake waliopo gerezani.
Neema Mghen akizungumza

“Tumekuja kuwaambia kuwa walipo si mwisho wa maisha yao. Ndoto zao bado zina thamani na wana nafasi ya kuanza upya. Wanapaswa kuendelea kuwa na ujasiri na kujiandaa kuwa wanawake imara watakapotoka hapa,” ameeleza Bi. Mghen.

Naye Mkuu wa Gereza la Kahama, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Bonis Njoka Gervas, ametoa shukrani kwa kundi hilo kwa msaada na faraja walioutoa, akieleza kuwa hatua hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa urekebishaji wa wafungwa.
Bonis Njoka Gervas akizungumza

“Wafungwa wanahitaji sana faraja na kutiwa moyo. Msaada kama huu unasaidia kuleta utulivu na amani gerezani huku ukiwajengea matumaini wanapokuwa wakisubiri kumaliza vifungo vyao au kesi zao,” amesema.

TAMASHA LA MWANAMKE CHUMA 2026 

Maandalizi ya Tamasha la Mwanamke Chuma 2026 yamekamilika, ambapo tukio hilo kubwa linatarajiwa kufanyika Jumamosi, Aprili 11, 2026 katika Ukumbi wa Malex Hall, Kahama kuanzia saa 11 jioni.

Tamasha hilo, linaloandaliwa na Kituo cha Redio cha Gold FM, limejipambanua kama jukwaa muhimu la kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi kupitia elimu, mitandao na fursa mbalimbali.
Tamasha la mwaka huu linatarajiwa kupambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo msanii mkongwe wa muziki wa Taarab, Mzee Yusuph, huku mtaalamu wa maendeleo ya familia na uchumi, Dkt. Chris Mauki, akitoa mada maalum zitakazolenga kuwainua wanawake na jamii kwa ujumla. 

Aidha, shughuli hiyo itasindikizwa na ucheshi na uchangamshi kutoka kwa MC maarufu, Dkt. Kumbuka.

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ambaye atahitimisha rasmi tamasha hilo linalotarajiwa kuvuta washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa.

Mbali na burudani na elimu, tamasha hilo pia litahusisha utoaji wa tuzo kwa wanawake waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali, ikiwemo ubunifu, ujasiriamali, ushonaji, upishi, saluni pamoja na wanawake wenye ushawishi chanya katika jamii.

Kwa mujibu wa waandaaji, tamasha hilo ni zaidi ya burudani, ni jukwaa la kuibua vipaji, kuhamasisha uthubutu na kuimarisha mchango wa mwanamke katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Wananchi wa Kahama na maeneo jirani wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo muhimu ambalo linabeba ujumbe wa matumaini, uthubutu na nguvu ya mwanamke wa kisasa.









Share this

Related Posts

Previous
Next Post »