MAFUTA KUPANDA BEI, SERIKALI YAAHIDI SULUHISHO KWA WANANCHI

April 01, 2026


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli na mafuta mengine ili kuhakikisha bei zake zinaendelea kuwa himilivu, licha ya kuwepo kwa changamoto za kiusalama za kikanda na kimataifa ikiwemo za Mashariki ya Kati zilizosababisha kupanda kwa bei ya mafuta nchini.


“Tumeona bei zimeanza kupanda, tutakaa ndani ya Serikali kuweza kuhakikisha tunakabiliana nalo vipi, ili wananchi wananchi wanaendelea kupata mafuta kwa bei wanazoweza kumudu na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha,” amesema Dkt. Mwigulu 

Amesema hayo leo, tarehe 1 Aprili 2026, wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2026/2027 Bungeni, jijini Dodoma. 


Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeendelea kusimamia mifumo ya kuagiza, kuhifadhi na kusambaza mafuta, pamoja na kuongeza uwezo wa kupokea na kuhifadhi mafuta katika bandari za Dar es Salaam na Mtwara.


Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa ghala la kupokea na kuhifadhi mafuta lenye uwezo wa tani 308,110 katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 30.



Ameongeza kuwa miundombinu ya kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Mtwara imeongezeka kutoka tani 29,280 hadi tani 110,221, hatua itakayowezesha kupokea meli yenye shehena ya tani 30,000.


Kwa upande mwingine, amesema Serikali imeendelea kuhakikisha ongezeko la matumizi ya gesi asilia, Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, mtandao wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika viwanda, taasisi na makazi umeongezeka hadi kilomita 243.6, ikilinganishwa na kilomita 184.8 hapo awali.


Kadhalika, amezielekeza Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Nishati kushirikiana kuandaa viwango msawazo (specifications) vitakavyotumika katika mahitaji ya vyombo vya moto vya Serikali, pamoja na kujenga miundombinu ya kutosha ili kuwezesha vyombo hivyo kuanza kutumia gesi asilia iliyoshindiliwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »