SHULE YA VIZIWI NJOMBE YAHAMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

March 16, 2026


Na Mwandishi Wetu,Njombe

SHULE ya Sekondari ya Viziwi mkoani Njombe imetekeleza agizo la Serikali la kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuepukana na madhara ya kiafya yanayosababishwa na moshi wa nishati chafu.

Akizungumza wakati wa ziara ya timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati iliyotembelea shule hiyo kukagua utekelezaji wa agizo hilo, Mjiolojia kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia,  Nsajigwa Maclean, amesema shule hiyo imefanikiwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya kampeni ya utoaji wa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Njombe.

 Maclean amefafanua kuwa matumizi ya nishati mbadala kama gesi, majiko banifu na umeme yana mchango mkubwa katika kupunguza uharibifu wa misitu unaotokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Aidha, amesema moshi unaotokana na matumizi ya nishati za jadi umekuwa ukichangia kusababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji kwa wapishi na wanafunzi, hivyo matumizi ya nishati safi yanasaidia kulinda afya pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia shuleni.

Amezipongeza shule ambazo tayari zimeanza kutumia nishati safi ya kupikia, akisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kulinda mazingira na kuboresha afya za watumiaji.

Amesema Wizara ya Nishati itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha taasisi mbalimbali, ikiwemo shule, hospitali na magereza, kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia nishati safi na salama kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Viziwi,  Rosemary Mbuya, amesema kufuatia agizo la Serikali, shule hiyo iliamua kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kutokana na gharama kubwa za upatikanaji wake.

“Gharama ya kununua kuni na mkaa ilikuwa kubwa sana, na mara nyingi tulilazimika kuvifuata mbali. Pia wapishi wetu walikuwa wakikumbwa na changamoto za kiafya mara kwa mara kutokana na moshi,” amesema Mbuya.

Ameongeza kuwa tangu kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, kumekuwa na maboresho makubwa katika ufanisi wa shughuli za jikoni pamoja na afya za wapishi.

 Amesema matumizi ya gesi yamepunguza muda wa kupika chakula kwa wanafunzi na kupunguza gharama zilizokuwa zikitumika kununua kuni na mkaa mara kwa mara.

Mwalimu Mbuya pia amebainisha kuwa hatua hiyo imechangia kulinda mazingira kwa kupunguza utegemezi wa ukataji wa miti kwa ajili ya kuni.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »